
Waandaaji wa kampeni kubwa ya mshikamano wa kimataifa wameweka wazi mpango wa juhudi kubwa zaidi ya kiraia kwa njia ya bahari, kwa lengo la kuvunja mzingiro wa muda mrefu uliowekwa na utawala wa Israel dhidi ya Gaza. Msafara huo wa baharini unatarajiwa kuanza safari katikati ya Aprili 2026.
Mpango huo unaoendeshwa na Global Sumud Flotilla, pia ukijulikana kama Freedom and Sumud Flotilla, ulitangazwa kupitia taarifa na mikutano ya waandishi wa habari, ikiwemo mkutano uliofanyika Istanbul kwa washiriki kutoka Uturuki siku ya Jumatano.
Dhamira hii inaunganisha juhudi za awali za Freedom Flotilla Coalition na msafara wa Sumud Convoy, ikijengwa juu ya majaribio ya mwaka 2025 ambayo yalizuiwa na vikosi vya majini vya Israel.
Kwa mujibu wa waandaaji, flotilla hiyo itaanza safari kutoka bandari kadhaa za Mediterania, ikianza na Barcelona, Uhispania mnamo Aprili 12, kisha bandari za Italia na Tunisia siku chache baadaye.
Waandaaji wanasema idadi kubwa ya meli, baadhi ya taarifa zikisema hadi 200, ingawa vyanzo rasmi vinasema zaidi ya meli 100, itafanya iwe vigumu kwa vikosi vya Israel kuuzuia msafara wote kwa wakati mmoja.
Inatarajiwa kuwa maelfu ya washiriki kutoka takribani nchi 150 watahusika, kwa uratibu na msaada wa zaidi ya mashirika 200 ya kiraia duniani kote.
Msafara huu umeelezwa kuwa ni juhudi ya wananchi pekee, isiyo ya kiserikali, bila udhamini rasmi wa serikali au mashirika makubwa ya kimataifa. Msisitizo mkubwa katika safari ya Aprili utakuwa ni msaada wa kibinadamu na kitaaluma.
Msafara huu unapanga kubeba zaidi ya wahudumu 1,000 wa afya, wakiwemo madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa tiba, pamoja na wahandisi, wanasheria, wachunguzi wa uhalifu wa kivita, na vifaa muhimu kama dawa za kuokoa maisha.
Msisitizo huu, kwa mujibu wa waandaaji, ni mwitikio wa uharibifu wa kimfumo wa miundombinu ya afya ya Gaza, unaoendelea sambamba na vita na vizuizi vikali vya upatikanaji wa misaada.
Kampeni pana ya Global Sumud ya Majira ya Kuchipua 2026 pia inajumuisha misafara ya misaada ya nchi kavu, ikihusisha mamia ya malori, kwa awamu mbalimbali, ili kuikabili mzingiro kupitia njia tofauti na kusisitiza haki ya Wapalestina ya kusafiri kwa uhuru na kufikia maji yao ya eneo.
Waandaaji wanauelezea mpango huu kama changamoto ya moja kwa moja, ya amani (bila vurugu), dhidi ya mzingiro wa majini wa Israel uliowekwa tangu mwaka 2007 na kuimarishwa zaidi katika vipindi vya vita.
Wanasema Israel imeweka mzingiro haramu ambao umechangia maafa makubwa ya kibinadamu, ikiwemo hatari ya njaa, uhamishaji wa watu kwa wingi, na mateso makubwa kwa wakazi wa Gaza.
Kwa kuhimiza dhana ya sumud (kusimama imara kwa subira na heshima), kundi hilo linatoa wito wa mshikamano wa kimataifa ili kukomesha mauaji ya halaiki, uvamizi, na ukandamizaji unaoendelea.
3496579