IQNA

Maisha ya Shahidi Imam Khamenei kwa mtazamo wa Aya ya Qur’ani Tukufu

17:54 - May 11, 2026
Habari ID: 3482228
IQNA – Msomi mmoja wa Kiislamu kutoka India amesema kuwa shakhsia au haiba maisha ya kiongozi aliyeuawa wa Mapinduzi ya Kiislamu yanaweza kutazamwa kwa kurejelewa katika aya ya Qur’ani.

Kwa mujibu wa Ahmad Reza Rizvi Zararah, mkuu wa tawi la Qom la Majlis Ulema-e-Hind, haiba ya  Shahidi Ayatullah Seyed Ali Khamenei imeelezwa katika makala yake kuwa mfano wa maana ya kauli ya Qur’ani isemayo: “Ashshida’a ‘ala al-kuffar ruhama bainahum” (wakali dhidi ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao).

Ameandika kwamba Qur’ani Tukufu si kitabu cha mwongozo pekee kwa jamii ya wanadamu, bali pia ni mfumo kamili wa maisha. Kwa mujibu wa maelezo hayo, Qur’ani inaeleza sifa za waumini wanaounda jamii iliyo sawa, na miongoni mwa sifa hizo ni ile iliyotajwa katika aya ya 29 ya Surah Al-Fath:

“Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye ni wakali dhidi ya makafiri, na wenye kuhurumiana wao kwa wao.”

Makala hiyo inaeleza kuwa katika historia ya Uislamu kumekuwapo watu ambao walidhihirisha maana ya aya hiyo katika maisha yao, na kwamba kiongozi huyo alihesabiwa na mwandishi kuwa miongoni mwa mifano hiyo.

Huruma kwa waumini

Kwa mujibu wa makala hiyo, upande mmoja wa haiba yake ulikuwa upole wa moyo na mapenzi kwa Umma. Mwandishi anasema kuwa aliutazama Umma si kama mkusanyiko wa kisiasa au kijamii tu, bali kama familia kubwa.

Makala hiyo inaongeza kuwa hotuba zake zilikuwa na lugha ya upendo, sauti ya huruma, na mwenendo wa ikhlasi. Aidha, inaelezwa kuwa alionesha mshikamano na wanazuoni, wanafunzi, vijana, wapiganaji, na watu wa tabaka dhaifu.

Mwandishi pia anasema kuwa mara nyingi aliwahimiza vijana kuwa na matumaini, kujiamini, na kuwa na uelewa wa dini. Kwa mujibu wa maelezo hayo, aliamini kuwa nguvu halisi ya Umma imo kwa vijana wake walio macho na wenye imani.

Kadhalika, makala hiyo inasema kuwa kwa mtazamo wake, msingi wa jamii ya Kiislamu ulipaswa kujengwa juu ya mapenzi, udugu, na ushirikiano wa pamoja, huku akihimiza kuepuka migawanyiko na kusisitiza umoja wa Kiislamu.

Msimamo dhidi ya maadui wa Uislamu

Makala hiyo inaeleza kuwa ikiwa upande mmoja wa haiba yake ulikuwa wa upole na huruma, upande mwingine ulikuwa wa ushujaa na uthabiti. Inaelezwa kuwa inapohusu Uislamu, Umma, na haki za wanaodhulumiwa, alichukua misimamo iliyoonekana kuwa ya wazi na thabiti.

Kwa mujibu wa mwandishi, alionesha upinzani dhidi ya kiburi, dhulma, na ukoloni, na hilo ndilo linalohusishwa na sehemu ya aya inayosema: “wakali dhidi ya makafiri.”

Makala hiyo inaongeza kuwa aliamini kwamba Umma wa Kiislamu ukitaka kuhifadhi heshima na uhuru wake, unapaswa kushikamana na msimamo imara badala ya kunyenyekea mbele ya nguvu za uongo.

Maisha ya jihadi na uongozi wa fikra

Kwa mujibu wa makala hiyo, maisha yake hayakujikita katika hotuba za kimawazo pekee, bali pia katika vitendo. Mwandishi anataja maisha yake kama ya juhudi, mwamko, na huduma kwa dini.

Inaelezwa pia kuwa aliwasilisha ujumbe wa mwamko wa kifikra kwa Umma, huku akisisitiza kuwa Uislamu ni dini hai na yenye harakati, isiyoruhusu kunyamaza mbele ya dhulma na uonevu.

Makala hiyo inasema kuwa uongozi wake uliwapa wengi roho ya kujiheshimu, uhuru, na msimamo. Aidha, mwandishi anaeleza kuwa hata katika mazingira magumu, aliweza kuonesha njia sahihi kwa Umma, na kwamba aliwahimiza Waislamu kusonga mbele kwa elimu, hikima, na ufahamu wa kina wa dini, si kwa hisia pekee.

Bila shaka, kwa mujibu wa maelezo hayo, haiba ya Kiongozi Mkuu ilitazamwa kama tafsiri hai ya kauli ya Qur’ani: “ashiddā’u ‘ala al-kuffār ruḥamā’u baynahum” (wakali dhidi ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao), na ujumbe wake unaelezwa kuwa unaendelea kuwafundisha waumini kote duniani kuhusu heshima, umoja na uthabiti.

3497415

Habari zinazohusiana
captcha