IQNA

Tarjuma mpya ya Qur’an Tukufu kwa Kiukreni  

19:17 - May 19, 2026
Habari ID: 3482261
IQNA-Nchini Ukraine, Uislamu una historia ya muda mrefu inayorudi hadi karne ya 10, na leo hii unaendelea kuwepo kama sehemu muhimu ya jamii ya kidini nchini humo.

Ingawa Wakristo ndio wengi, Waislamu pia wana idadi inayoonekana, hasa katika maeneo ya Crimea na miji mikubwa kama Kyiv, Kharkiv na Dnipro. Katika muktadha huo, jumuiya ya Waislamu wa madhehebu ya Mashia imeendelea kukua, hasa baada ya kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti, na imeanza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kidini, ikiwemo da’wah, maombolezo ya Ashura, na tafsiri za maandiko ya Kiislamu kwa lugha ya Kiukreni.

"Kwa mujibu wa takwimu fulani, takriban Waislamu 100,000 nchini Ukraine ni wa madhehebu ya Kishia. Mashia hawa nchini humo kwa kiasi kikubwa ni wahamiaji kutoka Jamhuri ya Azerbaijan, Iran, Kazakhstan, na Uzbekistan.

Baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti na Ukraine kupata uhuru wake, Mashia nchini humo walianza shughuli zao za da’wah (kulingania dini), na baadhi ya raia wa Ukraine walisilimu na kuwa wafuasi wa madhehebu ya Shia au Ahlul-Bayt (AS). Kwa miaka mingi sasa, Mashia nchini Ukraine wamekuwa wakitekeleza ibada za maombolezo ya Siku ya Ashura."

Miongoni mwa hatua muhimu za jumuiya hiyo ni uzinduzi wa tarjuma ya Qur’an Tukufu kwa lugha ya Kiukreni. Tarjuma  hii ilichapishwa mwaka 2021 katika miji ya Kyiv na Kharkiv, na inachukuliwa kuwa tarjuma au tafsiri ya nne kamili ya Qur’ani katika lugha hiyo. Mradi huo uliendeshwa na timu ya wasomi wanne chini ya uongozi wa Namik Babakhanov, mhubiri Mukiukreni mwenye asili ya Azerbaijan na mwenye elimu ya juu katika Masomo ya Kiislamu kutoka Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.

Tarjuma hii ilitegemea matini ya Kiarabu pamoja na tafsiri nyingine za Kiajemi, Kituruki na Kirusi. Hata hivyo, watafiti wamebainisha kuwa tarjuma hiyo inaegemea zaidi sana tarjuma ya Kirusi ya Magomed-Nuri Osmanov (1924–2015), jambo linaloibua hoja za kitaaluma kuhusu usahihi na uhalisia wa tarjuma ya moja kwa moja kutoka Kiarabu. Wakati huo huo, tarjuma hiyo inaonekana kubeba mtazamo wa Kishia, hasa katika baadhi ya masuala ya fiqhi kama vile udhuu katika Qur’ani Tukufu Sura Al Maidha aya ya 6, ambako hukumu ya kuifuta miguu kwa mkono wenye unyevunyevu imewekwa kwa namna inayolingana na fiqhi ya Kishia.

Pamoja na hayo wataalamu wameona kuwa tarjuma hii ina mapungufu kadhaa, hasa pale inapotegemea sana tarjuma ya pili badala ya Kiarabu asilia.

Kwa jumla, mradi huu ni muhimu kwa sababu unaonyesha juhudi za jumuiya ya  Waislamu wa madhehebu ya Shia  nchini Ukraine kuwasilisha Uislamu katika lugha ya taifa lao na kwa mtazamo wao wa kimadhehebu. Pia unaonyesha jinsi tafsiri za Qur’an zinavyoweza kuwa sehemu ya kazi ya da’wah, utambulisho wa kidini, na kubainisha mitazamo ya kifikra kati ya madhehebu mbalimbali ya Uislamu nchini humo.

3497514

Kishikizo: qurani tukufu ukraine
captcha