Vyanzo vya habari vya eneo hilo viliripoti kuwa mshambuliaji mwenye umri wa miaka 48 alimfuata mfanyakazi huyo, anayefahamika kwa jina la Sohail, katika Valley Fair Mall iliyoko West Valley City, akaanzisha mazungumzo mafupi na kumuuliza jina lake na kuhusu dini yake.
Kulingana na ripoti ya The Salt Lake Tribune, ikimnukuu Imam Shuaib Din, kiongozi wa Kituo cha Kiislamu cha Utah huko West Jordan ambaye amekuwa akiwasiliana na familia ya mhanga, mfanyakazi huyo alipogeuka kuchukua chupa ya maji, mshambuliaji alianza kumchoma visu.
Kituo cha utangazaji cha eneo hilo, KUTV, kilimtaja mshukiwa kuwa ni Peter Larsen, kikisema alitiwa nguvuni Jumatano baada ya polisi kufika kituoni hapo.
Kabla ya polisi kufika, watu waliokuwa karibu walimvamia mshambuliaji huyo, wakamdhibiti na kumnyang’anya kisu mkononi mwake, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama.
Polisi walisema kuwa mhanga na mshukiwa wote walilazwa hospitalini, mshukiwa akiwa amejeruhiwa baada ya kupigwa na mashuhuda wakati wa purukushani hiyo. Shirika la habari la Reuters pia liliripoti kuwa mhanga huyo yuko katika hali mahututi.
Kampeni ya kusaidia matibabu iliyoanzishwa kupitia mtandao wa GoFundMe kwa ajili ya mfanyakazi huyo imebainisha kuwa anahitaji upasuaji wa mikono, moyo, na mapafu. Mshukiwa amezuiliwa katika jela ya Jimbo la Salt Lake na amekataliwa dhamana.
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR), ambalo ni shirika kubwa zaidi la kutetea haki za Waislamu nchini humo, limelaani vikali shambulio hilo na kuyataka mamlaka ya umma kukataa na kukomesha lugha za uchochezi dhidi ya Waislamu.
“Shambulio hili la kutisha ni ukumbusho mwingine kuwa lugha za uchochezi dhidi ya Waislamu zina madhara halisi katika maisha ya watu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Kitaifa wa CAIR, Nihad Awad, katika taarifa yake.
“Wakati Waislamu wanaposhutumiwa mara kwa mara, kuchorwa kama tishio, au kutendewa kama watu wasiostahili haki sawa na utu, baadhi ya watu wenye fikra potofu bila shaka huchukua hatua kufuata chuki hiyo,” aliongeza.
CAIR ilisema kuwa ilirekodi malalamiko 8,683 ya ubaguzi dhidi ya Waislamu mnamo mwaka 2025, idadi ya juu zaidi iliyorekodiwa tangu kuanza kufuatilia visa vya namna hiyo mnamo mwaka 1996.
Muungano wa Kiraia wa Waislamu wa Utah (Utah Muslim Civic League) pia umelaani shambulio hilo kama uhalifu wa chuki, na kuwapongeza watu walioingilia kati kumsaidia mhanga.
3498269