IQNA

Kyrgyzstan: Nuru ya Qur’an sasa imewafikia waja wa Allah wenye ulemavu wa macho

16:28 - June 30, 2026
Habari ID: 3482422
IQNA – Kwa ndugu zetu Waislamu wenye ulemavu wa macho katika maeneo ya kusini mwa Kyrgyzstan, kizuizi sasa kimeondoka; Kitabu Kitukufu cha Allah kiko mikononi mwao, tayari kwa kusomwa na kutafakariwa.

Katika mfululizo wa hafla za kheri zilizojaa baraka katika mikoa ya Osh, Jalal-Abad, na Batken, nakala za Qur’an zilizochapishwa kwa mfumo wa Nukta Nundu au Braille zimegawiwa bila gharama yoyote kwa waja wa Allah wasioona au wenye ulemavu wa macho. Juhudi hizi adhimu zimeongozwa na Baraza la Uongozi wa Kiislamu wa Kyrgyzstan (DUMK), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya kuimarisha elimu ya dini kwa wote.

Katika matukio haya ya kutukuza Neno la Allah, waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Ulemavu wa Macho wa Kyrgyzstan, Jalaluddin Abdivaliev, Imamu wa msikiti wa “Yyman”, Nimatullo Ryskulov, pamoja na wawakilishi wa ngazi za juu wa Mahakama za Kadhi (kaziyats) katika mikoa husika.

Waandaaji wamesisitiza kuwa toleo hili mahususi litawawezesha ndugu zetu wenye ulemavu wa kuona kusoma Kitabu Kitukufu kwa uhuru, bila kutegemea mtu wa kuwasomea, na hivyo kujipatia maarifa ya dini kwa kujitegemea. Hii ni hatua muhimu katika kujenga mazingira ya usawa na kuipanua milango ya ustawi wa kiroho kwa waislamu wote, bila kujali changamoto za kimaumbile.

Tukio hili linakwenda sambamba na mkakati wa maendeleo uliowekwa na Mufti Aziret Abduaziz Qari Zakirov, ambaye amedhamiria kuondoa vikwazo vyote vinavyozuia upatikanaji wa elimu ya dini kwa wananchi wenye mahitaji maalum.

Kwa mtazamo wa kiuchambuzi, hatua hii ya DUMK siyo tu ugawaji wa vitabu, bali ni ujumbe mzito kuwa Qur’an ni mwongozo kwa walimwengu wote, na kwamba juhudi za makusudi zinaweza kuondoa giza na kuleta nuru ya elimu katika nyoyo za waumini, popote walipo.

3498028

captcha