Aya ya 207 ya Surah Al-Baqarah katika Quran Tukufu inazungumzia mtu anayeuza nafsi yake kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Wafasiri wengi wa Kiislamu wanaeleza kuwa aya hii inarejelea kitendo cha kulala katika kitanda cha Mtume (SAW) usiku wa Laylat al-Mabit.
"Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake."
Mfasiri maarufu wa Kisunni, Al-Tha'labi (aliyefariki mwaka 1025 Miladia), anasimulia kuwa wakati Mtume Muhammad (SAW) alipoamua kuhama kutoka Makka kwenda Madina, alimkabidhi Ali (AS) jukumu la kurejesha amana na kulipa madeni ya watu. Usiku wa kuondoka kwake kuelekea Pangoni Thawr, wakati makafiri walipomzingira nyumbani kwake, Mtume (SAW) alimuagiza Ali (AS) kulala kitandani pake akiwa amejifunika shuka lake.
Wakati huo, Mwenyezi Mungu aliwaambia Jibreel na Mika'il "Nimeanzisha udugu baina yenu na nimepanga kuwa mmoja wenu ataishi muda mrefu zaidi ya mwenzake. Ni nani kati yenu atakayejitolea muhanga kwa ajili ya mwenzake?”
Hakuna malaika aliyekuwa tayari kujitoa muhanga.
Ndipo Mwenyezi Mungu aliposema: "Sasa, Ali (AS) amechukua nafasi ya Mtume, tayari kujitoa muhanga kwa ajili yake. Shukeni duniani mkamlinde".
Jibreel alisimama kichwani mwa Ali, na Mika'il miguuni pake. Jibreel akasema: “Hongera ewe Ali! Kupitia wewe, Mwenyezi Mungu anajivunia mbele ya malaika.”
Ndipo aya hii ilipoteremshwa, ikielezea sifa za Ali (AS). Katika aya hii, "muuzaji" ni binadamu, "mnunuzi" ni Mwenyezi Mungu, "bidhaa" ni roho, na "malipo" ni radhi za Mwenyezi Mungu. Tofauti na aya nyingine ambapo thawabu za mkataba huu huonyeshwa kama Pepo ya milele au wokovu kutokana na Moto wa Jahannam, aya hii inaangazia radhi za Mwenyezi Mungu kama malipo makuu.
Aya hii inahitimishwa kwa hakikisho la upole wa Mwenyezi Mungu: “Na Mwenyezi Mungu ni mpole kwa waja wake.”
Mwanazuoni Ibn Abi al-Hadid (aliyefariki mwaka 1258 M) anasema kuwa kitendo cha kishujaa cha Ali (AS) usiku wa Laylat al-Mabit kinatambuliwa wote wanaofahamu historia ya Kiislamu. Anasema wasiokitambua kisa hiki ni wale wasio Waislamu au wale wasiokuwa na ufahamu wa kutosha.
Marejeo
- Musnad Ahmad ibn Hanbal, Juz. 1, uk. 348
- Siraat-e Ibn Hisham, Juz. 2, uk. 29
- Tarikh al-Yaqubi, Juz. 2, uk. 39
- Sharh Nahj al-Balaghah na Ibn Abi al-Hadid, Juz. 3, uk. 370
3491460