IQNA- Kiongozi Mkuu wa kidini wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq Ayatullah Sayyid Ali Sistani amesema, Papa Francis alikuwa na hadhi ya juu kiroho mbele ya mataifa mengi kutokana na mchango wake wa kipekee katika kuhimiza amani na kuvumiliana pamoja na kuonyesha mshikamano na watu wanaodhulumiwa duniani.
Ayatullah Sistani amesisitizia pia ulazima wa kufanyika juhudi za pamoja kwa ajili ya kuimarisha utamaduni wa kuishi pamoja kwa amani, kujiepusha na chuki na vitendo vya utumiaji nguvu, na kutilia mkazo thamani na tunu zinazokubaliwa na watu wote kwa msingi wa kuchunga haki na kuheshimiana wafuasi wa dini na mielekeo mbalimbali ya kifikra.