IQNA

Kusoma Qur’ani Kwenye Njia ya Arbaeen ‘Hakuna Mfano Wake,’ Asema Qari

23:09 - August 12, 2025
Habari ID: 3481073
IQNA – Qari kutoka Iran, Hamidreza Amadi-Vafa, amesema kuwa kusoma Qur’ani katika njia ya kutoka Najaf hadi Karbala wakati wa Arbaeen hujenga mazingira ya kiroho yasiyo na mfano katika nyakati nyingine za mwaka.

Arbaeen, ambayo mwaka huu itaadhimishwa tarehe 14 Agosti, ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani inayofanyika kila mwaka. Huashiria siku ya arobaini tangu Ashura, tukio la kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW).

Mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kutoka Iraq, Iran na maeneo mengine husafiri kwa miguu umbali mrefu kuelekea Karbala, palipo kaburi tukufu la Imam Hussein (AS), ili kushiriki katika ibada za maombolezo.

Iran hutuma msafara wa Qur’ani kila mwaka kuelekea Iraq kwa ajili ya tukio hili. Msafara huo huendesha ratiba za Qur’ani na dini kando ya njia ya matembezi ya Arbaeen, zikiwemo qiraa, adhani na tawasheeh.

“Qiraa ya Qur'ani katika njia ya kuelekea Haram ya mam Hussein (AS), huwa na hali ya kipekee ya kimaanawi,” Amadi-Vafa aliambia kipindi maalum cha Arbaeen cha Radio ya Qur’ani katika matangazo ya moja kwa moja kutoka barabara ya Najaf–Karbala. “Hii ni hisia adimu sana kutokea katika kipindi kingine cha mwaka.”

Amesema kuwa hali hiyo huonekana kuanzia mwanzo wa safari. “Unaweza kuona uaminifu na ikhlasi ya wafanyaziyara katika njia hii, ambayo kwa hakika ni njia ya mapenzi na muungano na Imamu mpenzi,” alibainisha.

“Kuanzia hatua za mwanzo, mahujaji hukaribishwa na watumishi wa Imam Hussein (AS), na matukio yasiyosahaulika hujitokeza, ambayo mtu sharti ayaone kwa macho yake mwenyewe,” alisema.

Amadi-Vafa, ambaye amekuwa akihudhuria hija ya Arbaeen kila mwaka tangu 2016, aliongeza kuwa Qur’ani imemletea nyakati za muunganiko wa kina wa kiroho. “Katika sehemu tunazosoma, baadhi ya mahujaji hunitambua kutokana na miaka iliyopita au kupitia matangazo ya televisheni na huja mbele kuonesha upendo na heshima zao,” alisema.

3494217

Habari zinazohusiana
Kishikizo: arbaeen qurani tukufu
captcha