IQNA

Elimu ya Qur’ani yaimarishwa kimuundo katika Jimbo la Sarawak, Malaysia

14:00 - March 31, 2026
Habari ID: 3482108
IQNA – Katika juhudi za kuinua umahiri wa kusoma na kuelewa Qur’ani Tukufu kwa mpangilio wa kitaasisi, Baraza la Kiislamu la Sarawak (SUC) nchini Malaysia linaendeleza upanuzi wa mtandao wa vituo vya “Rumah Ngaji,” likihama kutoka madarasa ya hapa na pale kwenda mpango ulioratibiwa katika ngazi ya jimbo zima.

Baraza hilo linaongeza juhudi za kuimarisha elimu ya Qur’ani kwa kupanua uanzishaji wa vituo vya “Rumah Ngaji” kote Sarawak, kwa lengo la kukuza jamii inayojua kusoma na kufahamu Qur’ani.

Rais wa baraza hilo, Datuk Misnu Taha, amesema kuwa hadi sasa jumla ya vituo 32 vya Rumah Ngaji vimesajiliwa, vikihusisha maeneo kama Lawas, Limbang na sehemu nyingine kadhaa, huku mipango ikiendelea kupanua huduma hizo katika maeneo zaidi.

Amesema vituo hivyo vya kujifunzia vinaanzishwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo surau (sehemu ndogo za ibada), misikiti, na hata majumba binafsi yaliyoandaliwa kwa vifaa vinavyofaa, ili kurahisisha kwa jamii za wenyeji kupata fursa ya kujifunza na kuielewa Qur’ani Tukufu.

Amesema: “Juhudi hizi zitaendelea kuimarishwa kwa msaada wa wadau mbalimbali ili Waislamu wengi zaidi katika Sarawak waweze kushiriki kwa uthabiti katika kujifunza Qur’ani. Tunataka vituo hivi viwe na nafasi muhimu katika kuboresha usomaji, ufahamu na mapenzi ya Qur’ani miongoni mwa jamii.”

Alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wanahabari wakati wa kupokea ziara ya heshima ya ujumbe wa Sarawak unaoshiriki katika Mkutano wa Kitaifa wa Usomaji na Uhifadhi wa Qur’ani 2026, uliofanyika katika Ghorofa ya 17 ya Majma’ Mall tarehe 30 Machi.

Ameeleza kuwa mwitikio wa jamii kwa programu zinazohusiana na Qur’ani umekuwa wa kutia moyo sana. Mfano ni hafla kubwa ya khatma ya Qur’ani iliyofanyika hivi karibuni mjini Lawas, iliyovutia washiriki wapatao 1,100.

Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa vituo hivi ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha maendeleo ya elimu ya Qur’ani katika Sarawak, sambamba na mpango wa kuanzisha Kituo cha Qur’ani cha Sarawak, ambacho kitakuwa taasisi kuu ya kuratibu programu zinazohusiana na Qur’ani katika jimbo hilo.

Aidha, Baraza la Kiislamu la Sarawak linaendelea na juhudi za kutafsiri Qur’ani katika lugha mbalimbali za makabila ya Sarawak ili kupanua uelewa wa ujumbe wake kwa jamii tofauti.

Amesema: “Hadi sasa tafsiri zimekamilika katika lugha za Iban, Bidayuh na Melanau, miongoni mwa nyinginezo, na juhudi hizi zitaendelea kuimarishwa ili watu wengi zaidi waweze kufahamu ujumbe wa Qur’ani.”

Wakati huo huo, vituo vya Qur’ani pia vinaweka mkazo katika ujumuishi kwa kutoa fursa za kujifunza kwa makundi maalumu, ikiwemo watu wenye ulemavu wa kuona kupitia maandishi ya Braille, pamoja na watu wenye matatizo ya kusikia.

Katika maendeleo yanayohusiana na hilo, Sarawak itatuma wawakilishi sita kushiriki katika Mkutano wa Kitaifa wa Usomaji na Uhifadhi wa Qur’ani 1447H/2026M, unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 13 hadi 18 Aprili katika jimbo la Terengganu.

349693

Habari zinazohusiana
Kishikizo: malaysia qurani tukufu
captcha