Hatua hii imekuja sambamba na maadhimisho ya Siku ya Miswada ya Kiarabu, siku inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 4 Aprili na taasisi mbalimbali katika nchi za Kiarabu, kwa kutambua thamani na urithi mkubwa uliomo katika miswada hiyo ya kale.
Baada ya kazi ya uhifadhi na urekebishaji kukamilika, makumbusho yamewasilisha tena moja ya nakala hizi za Qur’ani katika hali yake mpya. Nakala hiyo inaonesha uzuri wa sanaa ya uchapaji wa kale pamoja na hadhi ya juu ya miswada nadra ya Kiarabu.
Miongoni mwa hazina zilizopo katika makumbusho hayo ni mkusanyiko wa miswada adimu ya Kiarabu, ikiwemo Qur’ani nadra iliyopatikana katika Msikiti wa Sidi Ali Al‑Maliji. Qur’ani hiyo imeandikwa katika karatasi ya ubora wa hali ya juu, na baadhi ya sehemu zake zimerejeshwa baada ya kusafishwa kwa uangalifu na kukamilishwa kwa sehemu zilizokuwa zimepotea.
Makumbusho hayo pia yanahifadhi idadi kubwa ya turathi za Kiislamu, hususan miswada ya vitabu vya dini, elimu na historia. Baadhi ya sehemu za mkusanyiko huo huoneshwa kwa umma katika maonyesho maalumu yanayoandaliwa wakati wa sikukuu na matukio ya kidini na Kiislamu.
Makumbusho ya Kitaifa ya Ustaarabu wa Misri yalifunguliwa rasmi mwaka 2021 katika hafla kubwa iliyoshuhudia kuhamishwa kwa mumia 22 za wafalme wa kale kwenda katika eneo hilo. Vitu vya kihistoria vilivyohifadhiwa humo vinawakilisha urithi wa kimwili na wa kiroho wa Misri.
Kupitia makusanyo yake, makumbusho hayo huwasaidia wageni kuelewa safari ya ustaarabu wa Misri katika vipindi mbalimbali vya historia — kuanzia zama za kabla ya historia, hadi enzi za Misri ya kale, Wagiriki, Warumi, kipindi cha Wakopt (Wamisri Wakristo wa asili), enzi ya Kiislamu na nyakati za kisasa.
Taasisi nyingi katika ulimwengu wa Kiarabu huadhimisha Siku ya Miswada ya Kiarabu kila tarehe 4 Aprili, kwa kutambua umuhimu wa miswada hiyo ambayo hubeba hazina ya kielimu, kidini, kihistoria na kisayansi, pamoja na mchango wake katika kuimarisha utambulisho wa Kiarabu na urithi wa kitamaduni.
4344988