IQNA

Mushaf wa Rodossi: Nukta Muhimu katika Utambulisho wa Dini ya Algeria

15:15 - April 11, 2026
Habari ID: 3482134
IQNA – Mushaf wa Rodossi ni nakala ya Qur’ani ya kihistoria nchini Algeria inayotambulika kama nukta muhimu katika uundwaji wa utambulisho wa dini na ustaarabu wa taifa hili.

Kwa mujibu wa radioalgerie, Musahafu huu wa kihistoria ulichapishwa upya mwaka 2022 kwa agizo la Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa nchi hiyo.

Qur’ani hii, ambayo ilichapishwa nchini Algeria miongo kadhaa iliyopita, inachukuliwa kuwa marejeo muhimu katika kujifunza namna Qur’ani inavyofundishwa katika shule za Qur’ani na zawayah (madrasah za jadi za Qur’ani) nchini humo.

Mushaf wa Rodossi uliandamana na wapiganaji wa Mapinduzi ya Ukombozi wa Algeria katika harakati zao dhidi ya ukoloni wa Kifaransa, na katika historia ya kisasa ya nchi hiyo, umekuwa sehemu isiyotenganika ya urithi ambao Waalgeria wameutumia kulinda utambulisho wao wa kidini na kitaifa.

Mushaf huu, baada ya kupata umaarufu katika nchi za Ukanda wa Sahel, ulijulikana kama “Qur’ani ya Algeria” na ulisambazwa bure miongoni mwa mataifa ya eneo hilo ili kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kiroho kati ya Algeria na I Afrika.

Nakala hii ya Qur’ani pia inasambazwa katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu kama sehemu ya jitihada za Algeria kuhudumia Qur’ani na kueneza na kuimarisha maadili ya Kiislamu.

Musahafu wa Rodossi pia umesambazwa kwa ushirikiano na Wizara ya Mambo ya Nje miongoni mwa raia wa Algeria wanaoishi nje ya nchi, ikiwa ni juhudi za kuimarisha uhusiano na thamani za dini na utambulisho wa kitaifa.

Aidha, Wizara ya Masuala ya Kidini na Awqaf ya Algeria imekuwa ikitoa toleo hili bila malipo kwa wasomi na watu wenye maarifa.

Mwaka 2023, mushaf huu ulitolewa kwa toleo maalum katika muundo wa kawaida na pia katika maandishi ya Braille ili kuwajumuisha wenye uoni hafifu.

Kamati maalum chini ya uratibu wa Kamati ya Mapitio na Uchunguzi wa Qur’ani ya Algeria ilisimamia uchapishaji wa toleo la Braille la Qur’ani hii. Toleo la kawaida na la Braille la Musahafu wa Rodossi vimekuwa mabalozi wa Algeria katika ulimwengu wa Kiislamu na vinaonesha dhamira na kujitolea kwa Waalgeria katika kuitumikia Neno la Wahyi.

3497043

Kishikizo: algeria msahafu
captcha