
Ufalme wa Saudi Arabia unazidi kutegemea miundombinu mikubwa ya upozi na uwekaji vivuli iliyobuniwa mahususi kuwalinda wageni wa Mwenyezi Mungu (Dhuyufu-r-Rahman) dhidi ya joto kali na kurahisisha harakati katika maeneo matakatifu (Mashair).
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la SPA, kile kinachoonekana kwa mahujaji kama njia za kawaida zenye vivuli, kwa hakika ni sehemu ya juhudi kubwa za kihandisi zinazolenga kupunguza madhara ya joto wakati wa moja ya mkusanyiko mkubwa zaidi wa kidini duniani wa kila mwaka.
Katika miaka ya hivi karibuni, mamlaka husika zimepanua miradi mikubwa ya vivuli katika njia zinazotumiwa na watembea kwa miguu wengi zinazounganisha maeneo matakatifu. Wameweka mifumo ya kisasa ya mapaa (canopies) inayowakinga mahujaji na mionzi ya jua ya moja kwa moja, jambo linalosaidia kupunguza uchovu wa mwili wakati wa matembezi marefu kati ya ibada na nyengine.
Mkakati huu wa kukabiliana na joto pia umehusisha matumizi ya vifaa maalum vya sakafu vinavyoakisi mwanga na kunyonya joto kidogo ikilinganishwa na lami ya kawaida, hatua inayosaidia kushusha joto la ardhi wakati wa masaa ya mchana ambapo jua huwa kali zaidi.
Maeneo ya ziada ya kupumzikia yenye vivuli yameongezwa katika sehemu zenye msongamano mkubwa, yakiwaruhusu mahujaji kupumzika, kupata ubaridi, na kurejesha nguvu kabla ya kuendelea na safari yao ya ibada.
Mbali na vivuli vya kawaida, mamlaka zimeongeza matumizi ya mifumo ya kutoa ukungu wa maji kwa shinikizo la juu na kuongeza uoteshaji wa miti katika maeneo yenye mrundikano wa watu, ikiwa ni juhudi za kupunguza halijoto ya mazingira na kuboresha hali ya hewa.
Maandalizi yameimarishwa zaidi kwa ajili ya Hijja ya mwaka huu huku halijoto ikizidi kupanda katika ukanda huo, huku wataalamu wa hali ya hewa wakionya juu ya joto kali la mchana wakati wa siku kilele za ibada ya Hijja.
/3497582