IQNA

Msanii wa Dagestan na Tajiriba ya kiroho ya kuandika Qur’ani

12:03 - June 09, 2026
Habari ID: 3482344
IQNA – Suleiman Ashirlayev, msanii wa khatt kutoka Jamhuri ya Dagestan katika Shirikisho la Urusi, ameandika Qur’ani Tukufu nzima kwa maandishi ya Thuluth katika tajiriba aliyoiita ya kiroho.

Ashirlayev, ambaye ana zaidi ya miaka 35 ya uzoefu katika sanaa ya khatt ya Kiarabu na tazhib (upambaji wa maandishi ya Qur’ani kwa nakshi za dhahabu na mapambo ya Kiislamu), ameandika kwa mkono wake mwenyewe Qur’ani Tukufu nzima, hatua inayochukuliwa kuwa nadra katika eneo hilo katika miongo ya hivi karibuni.

Akitambulika Dagestan kwa kazi zake za kupamba na kuzipa nakshi misikiti, Suleiman anaheshimika katika duru za kidini na kitamaduni, na ametunukiwa heshima na tuzo mbalimbali za ndani kwa mchango wake wa muda mrefu katika kuhifadhi na kuendeleza sanaa ya khatt ya Kiarabu.

Katika mahojiano na Al Jazeera, Ashirlayev alisema kuwa uhusiano wake na khatt ya Kiarabu ulianza tangu utotoni, alipovutiwa kwa mara ya kwanza na umbo la herufi za Kiarabu.

Akikumbuka mojawapo ya kumbukumbu zake za awali, alisema:

“Nakumbuka kabla hata ya kuanza shule, nilipoona jina langu limeandikwa kwa mkono wa baba yangu, niliandika kwa penseli nyekundu. Nilikuwa na umri wa takriban miaka mitano, na tangu wakati huo mapenzi yangu ya kweli kwa khatt ya Kiarabu yalianza.”

Kwa miaka mingi, Ashirlayev amepamba misikiti kadhaa nchini Dagestan na maeneo mengine kwa sanaa yake, na alishiriki katika upambaji wa zaidi ya misikiti 100 kabla ya kuamua kuanza kuandika Qur’ani Tukufu nzima.

Msanii huyo alisema alitumia sehemu kubwa ya muda wake kuandika Qur’ani, kazi iliyochukua miezi minne na siku 19 za uandishi wa kila siku bila kukosa, isipokuwa nyakati za Swala na shughuli nyingine za lazima katika kijiji chake.

Ashirlayev haamini kwamba thamani ya misahafu iliyoandikwa kwa mkono inatokana tu na umri wake au nadra yake; bali anaamini kuwa sifa kuu iko katika ubora wa khatt na ustadi wa kufuata kanuni za kisanaa zilizowekwa na mabingwa wa khatt kwa karne nyingi.

Alisema kuwa watu wengi humletea misahafu ya kale ili aipime thamani yake, lakini kwa mtazamo wake, thamani halisi iko katika uzuri wa maandishi na uaminifu wa mwandishi kwa misingi na kanuni za sanaa hiyo tukufu.

Ashirlayev alichagua kuandika Qur’ani kwa mtindo wa Thuluth, mojawapo ya aina tata na zenye hadhi ya juu za khatt ya Kiarabu, ambayo hutumika pia katika mapambo na aya zilizoandikwa kwenye Kiswah (Sitarah ya Al-Kaaba Tukufu).

Alieleza kuwa alichagua mtindo huo kwa lengo la kuunda kazi itakayoakisi uhusiano wa watu wa Dagestan na eneo la Caucasus kwa ujumla wao na Qur’ani Tukufu.

3497771

captcha