IQNA

Hamas yalaani hatua ya Israel kupiga marufuku Adhana, yataka hatua kali zichukuliwe

17:23 - July 02, 2026
Habari ID: 3482428
ADHAN
IQNA-Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina (Hamas) iimelaani vikali uamuzi wa awali wa bunge la utawala wa Israel (Knesset) kupitisha muswada wa mrengo wa kulia wenye nia ya kupiga marufuku wito wa Sala ya Kiislamu (Adhana) kupitia vipaza sauti katika misikiti ya Mji Mkongwe wa al-Quds (Jerusalem) na maeneo mengine yote yaliyovamia na kukaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Hamas imeitaja hatua hiyo kuwa “uchokozi hatari” dhidi ya maeneo matakatifu ya Waislamu na jaribio la moja kwa moja la kufuta utambulisho wa Kiislamu wa Wapalestina.

Hamas imesisitiza kuwa muswada huo uliopendekezwa ni uvunjifu wa wazi wa uhuru wa kuabudu, na unakinzana na mikataba ya kimataifa inayolinda ibada na maeneo ya matakatifu.

Hamas imebainisha kuwa muswada huu ni sehemu ya mkakati mpana zaidi wa Israeli unaolenga kudhoofisha maeneo matakatifu ya Kiislamu, huku ukilenga kufuta kabisa utambulisho wa Kiarabu na Kiislamu katika ardhi za Palestina zilizovamiwa.

Harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestina imesema kuwa kuendelea kuibuka kwa sheria zinazolenga nembo za Kiarabu na Kiislamu ni ishara ya kukithiri kwa itikadi kali ndani ya sera za utawala wa Israel, na ni sehemu ya juhudi pana za kufanikisha “Uyahudishaji” wa mji wa al-Quds, hasa ikilenga Msikiti wa al-Aqsa na maeneo mengine matakatifu.

Hamas imesisitiza kuwa Adhana itaendelea kubaki kama nembo ya kudumu ya Uislamu na kipengele cha msingi cha utambulisho wa al-Quds na ardhi nyingine za Palestina. Imesisitiza kuwa sheria za Israeli hazitafanikiwa kuzinyamazisha sauti za misikiti wala kubadilisha historia na utambulisho wa ardhi ya Palestina.

Harakati hiyo  imetoa wito kwa Wapalestina, jumuiya za Kiarabu na Kiislamu, pamoja na mashirika ya dini na haki za binadamu, kuimarisha jitihada zao za kulinda eneo la Msikiti wa al-Aqsa na maeneo mengine matakatifu, kuunga mkono ustahimilivu (sumud) wa Wapalestina huko al-Quds, kupinga vizuizi vya uhuru wa ibada, na kuibua mjadala wa sera hizi za Israeli katika majukwaa ya kimataifa.

Mapema Jumatano, bunge la utawala haramu wa Israel ilipitisha “Muswada wa Muadhini” katika hatua ya awali ya kura, ambapo kura 50 ziliunga mkono na 36 kupinga.

Muswada huo unalenga kudhibiti matumizi ya vipaza sauti katika maeneo ya ibada, hasa misikiti, kwa kisingizio cha kupunguza kelele, kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya Israel.

Muswada huo uliungwa mkono na wabunge wa chama cha misimamo mikali cha Yisrael Beiteinu, chini ya uongozi wa Avigdor Lieberman, pamoja na wabunge wa chama cha Shas, hatua ambayo imezua ukosoaji mkali kutoka kwa wabunge wa chama cha Ra’am.

Licha ya kupitishwa katika usomaji wa awali, muswada huo bado unahitaji kupitia hatua nyingine tatu za usomaji bungeni kabla ya kuwa sheria kamili.

3498058

Habari zinazohusiana
captcha