
Mamlaka za Israel ziliwaruhusu Wapalestina 10,000 tu kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu kuingia katika Msikiti huo, ambao ni moja ya maeneo matakatifu zaidi ya Waislamu.
Watoto walio chini ya umri wa miaka 12, wanaume wenye zaidi ya miaka 55, na wanawake wenye umri wa miaka 50 au zaidi ndio walioruhusiwa na Wazayuni kuswali Masjidul Aqsa.
"Kuna watu milioni 3.3 wanaoshi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kwa hivyo kuruhusu 10,000 pekee kuswali Ijumaa hii ya kwanza ya Ramadhani ni tone baharini, na ni wachache tu ambao wameweza kuingia," Nour Odeh, ripota wa Al Jazeera amesema akiwa katika kituo cha upekuzi cha Qalandiya.
Katika miaka ya nyuma, hadi waumini 250,000 katika eneo hilo takatifu walikuwa wakifika katika Swala ya Ijumaa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Wapalestina wanawewekea vizuizi hivi katika hali ambayo, Walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada juzi walivamia tena Msikiti huo mtakatifu wa al-Aqsa na kufanya vitendo vya kichochezi dhidi ya Qibla hicho cha kwanza cha Waislamu.
Habari inayohusiana:
Msikiti wa al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds, na utawala pandikizi wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo; lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.
3496489