IQNA

Usajili wa Msafara wa Qur’ani wa Arbaeen wa Iran

10:44 - June 28, 2026
Habari ID: 3482413
IQNA – Muda wa usajili kwa wanaharakati na watumishi wa Qur’ani wanaotaka kushiriki katika Msafara wa Qur’ani wa Arbaeen wa Iran wa mwaka 2026 umeongezwa hadi Jumanne, tarehe 30 Juni.

Uamuzi wa kuongeza muda huo ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Shughuli za Qur’ani chini ya Makao Makuu ya Utamaduni ya Arbaeen, kilichofanyika siku ya Jumamosi mjini Tehran.

Kikao hicho kilipitia programu za hivi karibuni za Qur’ani zilizopangwa kwa ajili ya msafara wa Arbaeen wa mwaka huu, na pia kujadili namna ya kuimarisha uratibu na mshikamano kati ya taasisi mbalimbali zinazoshiriki katika shughuli hizo.

Katika mkutano huo, wawakilishi wa taasisi tofauti zinazojishughulisha na shughuli za Qur’ani zinazohusiana na Arbaeen waliwasilisha mipango yao kwa ajili ya tukio lijalo.

Katika kikao hicho, iliamuliwa kwamba mwaka huu kituo cha kudumu cha wanaharakati wa Qur’ani kitaanzishwa katika miji ya Najaf na Karbala pamoja na katika njia ya Arbaeen inayounganisha miji hiyo miwili.

Maelezo ya ziada pamoja na taratibu za kuanzishwa kwa kituo hicho yatatangazwa katika mikutano ijayo.

Kwa mujibu wa mpango wa mwaka huu, msafara wa Qur’ani wenye washiriki 100 utatumwa Iraq wakati wa msimu wa Arbaeen ili kuendesha programu mbalimbali za Qur’ani katika maeneo tofauti.

Maadhimisho ya maombolezo ya Arbaeen, ambayo mwaka huu yatafanyika tarehe 4 Agosti, ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani.

Arbaeen huadhimisha siku ya arobaini baada ya Ashura,siku ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein (AS).

Kila mwaka, umati mkubwa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia huelekea katika mji wa Karbala, ambako kunapatikana haram tukufu ya Imam Hussein (AS), ili kushiriki katika ibada na maombolezo.

Mazuwar wengi, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri umbali mrefu kwa miguu kuelekea mji huo mtukufu.

Iran pia hutuma msafara maalumu wa Qur’ani unaojulikana kama Msafara wa Noor kwenda Iraq wakati wa msafara wa Arbaeen.

Wanachama wa Msafara wa Noor huendesha programu mbalimbali za Qur’ani na kidini, zikiwemo tilawa ya Qur’ani Tukufu, adhani , na nashid, katika njia ya Najaf hadi Karbala na maeneo mengine wakati wa matembezi ya Arbaeen.

3497999

Habari zinazohusiana
captcha