IQNA

Vituo vya Tiba vya Makka Viko Tayari Kuhudumia Mahujaji

10:52 - April 25, 2026
Habari ID: 3482160
IQNA – Ziara ya siku mbili ya kukagua vituo vya afya katika mji mtukufu wa Makka, ili kutathmini utayari wao kwa msimu ujao wa Hija, imekamilishwa na waziri wa afya wa Saudia.

Ziara hiyo iliyoongozwa na Fahad Al‑Jalajel inaonyesha umuhimu unaotolewa katika kuwapatia mahujaji huduma za afya zenye viwango vya juu, sambamba na malengo ya Mpango wa Mageuzi ya Sekta ya Afya.

Waziri amesisitiza kuwa kuimarisha miundombinu ya afya ya Makka ni kipaumbele cha juu, huku mipango ya uendeshaji ikilenga kupanua uwezo na kuunganisha huduma za kinga, tiba, na dharura.

Amesema kuwa mkakati huo unajumuisha kuinua uwezo wa kitabibu na kiteknolojia wa watumishi wa afya, pamoja na kuhakikisha uratibu mzuri katika sekta yote ya afya ili kushughulikia kesi zote kwa ufanisi wa hali ya juu na kuhakikisha usalama wa mahujaji wakati wa ibada.

Katika ziara hiyo, waziri alikagua hali ya uendeshaji ya vitengo vya dharura na wagonjwa mahututi, taratibu kwa ajili ya kushughulikia kesi nzito, na mifumo ya mwitikio wa haraka.

Aidha, alikagua mfumo wa pamoja wa amri na udhibiti, pamoja na kiwango cha uratibu na huduma za ambulansi, ili kuhakikisha mwitikio wa haraka na mzuri wakati wa msimu wa Hija.

Ukaguzi huu ni sehemu ya ufuatiliaji endelevu wa wizara kwa ajili ya kuhakikisha viwango vya juu vya usalama wa kiafya na uimarishaji wa huduma katika maeneo yote matukufu.

3497209

Kishikizo: hija saudi arabia makka
captcha