Uongozi wa kabari au Haram hiyo takatifu umeandaa mpango maalum na wa kina wa kuratibu maombolezo ya Muharram, hasa katika siku kumi za mwanzo za mwezi huu mtukufu.
Haidar al-Isawi, mmoja wa maafisa wa Idara ya Mfawidhi wa Haram ya Imam Ali (AS) amesema kuwa mpango huo unahusisha mapokezi ya wafanyaziara au Zuwwar na makundi ya waombolezaji ndani na nje ya viwanja vya haram, pamoja na kuratibu maandamano ya maombolezo na ibada ya kubeba tochi ya moto inayofanyika karibu na maqamu hiyo tukufu.
Aidha idara hiyo imetayarisha mpango wa kuwaunga mkono wahudumu wa huduma katika mitaa ya zamani ya Najaf, ikiwa ni pamoja na wanaotoa huduma za maji ya kunywa, barafu, feni za kupunguza joto, vifaa vya usafi, pamoja na chakula katika siku kumi za mwanzo.
Kwa mujibu wa Jafar al-Badiri, afisa mwingine wa eneo hilo takatifu, mpango huo unajumuisha pia shughuli mbalimbali kama vile ibada ya kuinua bendera tukufu, maandalizi ya kiusalama na huduma za lojistiki zinazohitajika wakati makundi ya waombolezaji wanaingia katika eneo hilo takatifu.
Amesema pia kuwa mikutano kadhaa ya uratibu imefanyika kati ya makundi ya waombolezaji ili kuondoa vikwazo na kurahisisha mienendo yao katika kipindi chote cha siku kumi za mwanzo za Muharram.
Aidha, al-Badiri ameongeza kuwa maandalizi pia yanajumuisha kuratibu ibada ya kubeba tochi za moto, ibada inayofanyika kila mwaka katika usiku wa 8, 9 na 10 wa Muharram – ikiwa ni miongoni mwa kilele cha ibada za huzuni na kumbukumbu.
Waislamu wa Kishia, pamoja na waumini wengine duniani kote, huadhimisha kila mwaka kuuawa kwa Imam Hussein (Alayhis Salaam) na watu wa familia yake, waliouliwa shahidi katika ardhi ya Karbala mnamo tarehe 10 Muharram (Ashura), mwaka 61 Hijiria, katika mapambano na majeshi katili ya Yazid bin Muawiya.
Kwa mwaka huu wa 2025, Siku ya Ashura itasadifu Jumapili, tarehe 6 Julai.
3493636