Sambamba na kutangaza siku tano za maombolezo ya umma nchini kwa mnasaba wa kuuawa shahidi mujahid mkubwa na mshika bendera wa Muqawama na mapambano, Hujjatul-Islam Sayyid Hassan Nasrullah, Ayatullah Ali Khamenei, siku ya Jumamosi alitoa ujumbe wa rambirambi kwa safu nzima ya Muqawama (mapambano ya Kiislamu) na Umma wa Kiislamu na kusema: "Msingi aliouanzisha huko Lebanon na kutoa mwelekeo kwa vituo vingine vya nguvu, hautatoweka kwa kumpoteza Sayyid mpendwa, bali kwa damu yake na mashahidi wengine wa tukio hili, utaimarika zaidi, na mapigo ya Muqawama kwenye kiwiliwili kilichochakaa na kinachoelekea kuzimu cha utawala wa Kizayuni yatakua shadidi zaidi."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kwamba Sayyid Hassan Nasrullah, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, amepata ujira wa miongo kadhaa ya Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na mashaka yake kupitia mapambano matakatifu na kusema: Sayyid Hassan Nasrullah ameuawa shahidi alipokuwa akijishughulisha na mipango ya kuwalinda watu wasio na makazi wa vitongoji vya Beirut na nyumba zao zilizoharibiwa na wapendwa wao waliouawa kwa kukatwakatwa vipande, kama alivyofanya kwa miongo kadhaa kuwatetea watu waliodhulumiwa wa Palestina, miji iliyonyakuliwa, vijiji na nyumba zao zilizoharibiwa na wapendwa wao waliouawa kwa umati.
Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa: Ulimwengu wa Kiislamu umepoteza shakhsia mkubwa, Kambi ya Muqawama imepoteza kinara adhimu, na Hizbullah imepoteza kiongozi asiye na kifani, lakini baraka za Jihadi yake ya miongo mingi itabakia siku zote.
Ijumaa iliyopita ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel zilitekeleza mashambulizi ya kigaidi katika makazi ya raia eneo la Dhahiya, kusini mwa Beirut, na kuua shahidi watu kadhaa akiwemo Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon.
3490068