IQNA

Ayatullah Khamenei atoa wito wa maandamano ya siku ya Quds yenye "kiwango cha hali ya juu" 

0:51 - March 28, 2025
Habari ID: 3480449
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amesema maandamano ya kimataifa ya Siku ya Quds, Ijumaa hii, "kwa msaada wa  Mwenyezi Mungu, yatakuwa moja ya maandamano bora, ya kupendeza zaidi, na yenye heshima zaidi."

"Siku ya Quds daima ni ishara ya umoja na nguvu ya taifa la Iran," amesema Kiongozi katika ujumbe wa televisheni usiku wa Alhamisi. 

"Aidha siku hii pia ni ishara kuwa taifa la Iran lina msimamo thabiti na  imara  katika malengo yake muhimu, ya kisiasa, na ya msingi, na halitaachana na kauli mbiu ya kuunga mkono Palestina." 

Ayatullah Khamenei katika ujumbe wake ameelezea maandamano ya Siku ya Quds kuwa ni moja ya  chimbuko la heshima kwa taifa la Iran. 

"Tangu miaka 46 iliyopita, wananchi wa Iran wakiwa katika saumu wamekuwa wakihudhuria maandamano ya Siku ya Quds katika hali mbalimbali za hewa, si tu katika miji mikubwa bali pia katika miji midogo na vijijini," amesema Kiongozi Muadhamu. 

Ayatullah Khamenei amesitiza kuwa umuhimu wa maandamano ya Siku ya Quds mwaka huu ni mkubwa zaidi kuliko miaka iliyopita. 

"Mataifa ya dunia yako upande wetu; wale wanaotujua wako upande wa taifa la Iran, lakini baadhi ya wanasiasa na serikali zinazotupinga zinaeneza propaganda dhidi ya taifa la Iran: wanajifanya kuna tofauti na kuna udhaifu. 

"Maandamano yenu ya Siku ya Quds yatasambaratisha hila zote hizi na kauli hizi za uongo," amesema Kiongozi Muadhamu katika hotuba yake kwa taifa la Iran.

Inafaa kuashiria hapa kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ni miongoni mwa urithi wa mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu), ambaye anaheshimiwa kama kiongozi wa kiroho na Waislamu duniani kote. 

Mnamo mwaka 1979, muda mfupi baada ya kuongoza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yalimpindua mtawala wa kiimla, Shah, aliyeungwa mkono na Marekani pamoja na Israel, Imam Khomeini aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa Quds ili Waislamu na wapenda haki kote duniani waweze kujitokeza katika siku hiyo katika maandamano na mijumuiko ya kuunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina sambamba na kulaani utawala wa Kizayuni wa Israel unaozikoloni na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina mbali na kutenda kila aina ya jinai na ukatili dhidi ya Wapalestina.

Mji wa al-Quds (Jerusalem) unachukuliwa kuwa nembo ya ukombozi wa Palestina kwani unatazamiwa kuwa mji mkuu wa nchi huru ya Palestina.

4273937

Habari zinazohusiana
captcha