Shughuli ya mazishi na kuaga baadhi ya mashahidi wa mashambulizi ya utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel imefanyika leo Jumamosi tarehe pili Muharram kuanzia katika maidani Engelab hadi maidani Azadi katika kalibu ya msafara wa mashahidi wa matabaka mbalimbali wakiwemo watoto, wanawake, wanasayansi, makamanda na mashahidi wengineo.
Iran imefanya mazishi ya mashahidi hawa tajwa waliouawa katika mashambulizi ya siku 12 ya Israel na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Marasimu ya leo Tehran ya kuwaaga mashahidi hao yalianza mbele ya lango kuu la Chuo Kikuu cha Tehran, eneo ambalo siku zote limekuwa kitovu cha mapambano na kuwaaga mashahidi. Leo, wananchi wa Iran wanaume kwa wanawake, wazee kwa vijana wamemiminika mitaani wakiwa na mioyo yenye huzuni lakini yenye ujasiri ili kubeba miili safi ya mashahidi mabegani mwao.
Kuanzia asubuhi na mapema leo Jumamosi, eneo la maidani Engelab lilifurika umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika kwenye eneo la tukio wakiwa wameinua juu bendera nyekundu yenye maneno "Labaik Ya Hussein (AS)."
Mohsen Mahmoudi, Mkuu wa Baraza la Uratibu wa Maendeleo ya Kiislamu la Tehran ameitaja siku ya leo kuwa siku ya kihistoria kwa Iran ya Kiislamu na Mapinduzi.
Miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi ya Israel na Marekani ni Meja Jenerali Muhammad Bagheri Mkuu wa Majeshi ya Iran.
Ikumbukwe kuwa baada ya shughuli hii ya mazishi, miili hiyo ya mashahidi wa mashambulizi ya utawala haramu wa Kizayuni itazikwa katika baadhi ya makaburi ya Imamzadeh hapa Tehran, katika makaburi ya Behesht-e-Zahra na katika miji mingine hapa nchini.
3493609