Hafla hiyo, ambayo ilijaa huzuni na matumaini kwa wakati mmoja, ilihudhuriwa na maulamaa, familia za mashahidi, na viongozi wa kijamii na kidini. Kusomwa kwa aya hizo tukufu kulilenga kuimarisha roho ya subira, mapambano na tawakkul kwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Waislamu wanaokumbwa na dhulma. Aya hizo za Surah Al-Imran, miongoni mwa nyingine, zinaelekeza waumini kuendelea kushikamana na haki hata wanapopitia mitihani mikubwa, zikikumbusha kwamba ushindi wa kweli uko kwa wale waliodumu katika subira, istikama na kumtegemea Allah peke yake.
Kwa mujibu wa waratibu wa hafla hiyo, tukio hili pia lilikuwa njia ya kuonyesha mshikamano wa Ummah wa Kiislamu dhidi ya ubeberu wa kimataifa, sambamba na kulaani mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na maadui wa Uislamu katika maeneo kama Iran, Palestina, na sehemu nyingine za dunia.
Matamshi ya washiriki yalisisitiza kuwa damu ya mashahidi haitapotea bure, na kuwa mapambano ya Kiislamu dhidi ya dhulma na ukoloni mamboleo yataendelea kwa njia zote halali, za kisiasa, kijamii na kiroho.
138. Hii ni bayana kwa watu wote, na ni uwongofu, na mawaidha kwa wachamngu.
139. Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa juu mkiwa ni Waumini.
140. Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu wengine yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu, ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu;
141. Na pia ili Mwenyezi Mungu awasafishe walio amini na awafutilie mbali makafiri.
142. Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawapambanua wale miongoni mwenu walio pigana Jihadi, na hajawapambanua walio subiri?
143. Na nyinyi mlikuwa mkitamani mauti kabla hamjakutana nayo. Basi sasa mmekwisha yaona na huku mnayatazama.
144. Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwisha pita kabla yake Mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakaye geuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanao mshukuru.
145. Na haiwezi nafsi kuwa ife ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyo andikwa ajali yake. Na mwenye kutaka malipo ya duniani tutampa; na mwenye kutaka malipo ya Akhera tutampa. Na tutawalipa wenye kushukuru.
146. Na Manabii wangapi walipigana na pamoja nao Waumini wengi wenye ikhlasi! Hawakufanya woga kwa yaliyo wasibu katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakuwa wanyonge. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wanao subiri.
147. Wala kauli yao haikuwa ila ni kusema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie madhambi yetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu, na isimamishe imara miguu yetu na utunusuru tuwashinde kaumu ya makafiri.
148. Basi Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na bora ya malipo ya Akhera. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema.
149. Enyi mlio amini! Ikiwa mtawat'ii walio kufuru watakurudisheni nyuma, na hapo mtageuka kuwa wenye kukhasiri.
150. Bali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wenu, naye ndiye bora wa wasaidizi.
3480927