Rais Masoud Pezeshkian ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, akijibu wasiwasi wake kuhusu hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kusimamisha ushirikiano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
Huku akikosoa mienendo ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kwa kuwasilisha ripoti zisizo sahihi kuhusu faili la nyuklia la Iran na pia kwa kutolaani mashambulio dhidi ya vituo vya nyuklia vya Jamhuri ya Kiislamu, kinyume na sheria zote zilizopo, Rais Pezeshkian ameongeza kwamba: "Leo, maoni ya serikali, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na taifa la Iran ni kwamba Mkurugenzi Mkuu wa IAEA meachukua hatua za kiupendeleo dhidi ya Iran licha ya ushirikiano mkubwa wa nchi yetu, na mienendo hiyo hatukubaliano nayo kabisa."
Ameongeza kuwa, hatua ya Bunge la Iran ya kusitisha ushirikiao na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, ambacho imetokana na matakwa ya wananchi wa Iran, pia ni jibu kwa mienendo hiyo isiyo ya haki, isiyojenga na yenye uharibifu ya Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo.
Akisisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, licha ya kusisitiza mara kwa mara na kuthibitisha kwamba haina nia ya kuunda silaha za nyuklia, na vilevile kukaribisha mazungumzo ili kutatua sutafahamu na madai yaliyotolewa kuhusu shughuli zake za kuzalisha nishati ya nyuklia, imeshambuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel ikiwa kwenye mazungumzo na Wamarekani, kwa idhini na uungaji mkono wa Washington. Rais amesema: "Inasikitisha kwamba, jinai hii imepelekea kuuawa shahidi wanasayansi na makamanda kadhaa wa jeshi; na jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, badala ya kukemea na kulaani jinai hiyo, wanaodai kutetea haki za binadamu na sheria za kimataifa wamejaribu kuhalalisha kitendo hicho cha kinyama na kinyume cha sheria cha utawala wa Kizayuni na Marekani."
Rais Pezeshkian amesema kuwa, pale Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki anapopuuza kanuni za shirika hilo la kimataifa na kukataa kulaani mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni jambo lisilo na mantiki kutarajia nchi wanachama ziheshimu sheria za wakala huo.
Rais Pezeshkian amesema kuwa, swali zito la taifa la Iran katika hali ya hivi sasa ni kwamba: Kwa kuzingatia tajiriba za sasa, iwapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, kuna hakikisho gani kwamba mitambo ya nyuklia ya nchi yetu haitashambuliwa tena?
Katika mazungumzo hayo ya simu, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema kwamba Paris ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kulaani mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kwamba alitamka waziwazi suala hilo kwa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Macron amesema: "Pia tunaelewa na kuridhia misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu utekelezwaji sahihi na sawia wa sheria za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, na tunatilia mkazo kuendelea kwa ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wakala huo, hata ndani ya mfumo mpya, na vilevile kuendelezwa mchakato wa mazungumzo na nchi za Ulaya."
4291809