IQNA

Meya wa New York Anukuu Qur’ani na Mafundisho ya Kiislamu Kutetea Agizo la Kulinda Wahamiaji

11:51 - February 08, 2026
Habari ID: 3481900
IQNA – Meya wa Jiji la New York, Zahran Mamdani, ametetea agizo lake linaloweka mipaka kwa ukamataji unaofanywa na maafisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE), akieleza kuwa ulinzi wa wahamiaji si suala la kisera pekee, bali ni wajibu wa kimaadili unaochochewa na mafundisho ya Qur’ani Tukufu na Hijra ya Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake) kwenda Madina.

Wakati mjadala kuhusu sera za uhamiaji nchini Marekani ukizidi kushika kasi, Mamdani amejitokeza hadharani kutetea amri hiyo ya kiutendaji inayodhibiti ukamataji unaofanywa na ICE, akitumia misingi ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW) katika kuwasilisha ujumbe wake wa kuwatetea wahamiaji.

Mamdani alisisitiza kuwa simulizi la hijra hutukumbusha kwa hakika kwamba Mtume Muhammad (SAW) naye pia alikuwa mgeni alipolazimika kuondoka Makka, kabla ya kupokelewa kwa ukarimu mjini Madina.

Aliongeza kuwa simulizi hii inapaswa kuwa dira ya kimaadili kwa sera za nyakati hizi, akiwataka wenye mamlaka kuweka ustawi wa binadamu mbele ya taratibu kavu za kiutawala.

Mamdani alinukuu Aya Tukufu kutoka Suratul Nahl katika Qur’ani Tukufu isemayo: “Na wale waliohama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhulumiwa, bila shaka tutawakalisha duniani makazi mema.”

Alibainisha kuwa misingi hiyo ya Kiislamu inaweza kutafsiriwa katika sera halisi zinazohakikisha ulinzi na ujumuishi kwa wageni na wahamiaji, akisisitiza kwa kusema: “Na tuweke matarajio mapya kuhusu nafasi ya manispaa, ambapo mamlaka yatatumika kwa upendo, ujumuishi na ulinzi.”

Meya wa New York aliishutumu Idara ya ICE kwa kusambaza “hofu” miongoni mwa wahamiaji na kutekeleza vitendo alivyovitaja kuwa “vya kikatili na vinavyotikisa dhamiri.”

Mamdani alisema kuwa maafisa wa uhamiaji wa serikali ya shirikisho “wanawatoa watu kwa nguvu ndani ya magari yao, wakionesha silaha mbele ya raia wasio na silaha, na kuvunja familia kwa ukatili.”

Aliyataja sera za uhamiaji za serikali ya shirikisho kuwa ni “shambulio la moja kwa moja dhidi ya maadili ya kibinadamu na ya kidini,” akisisitiza kuwa vitendo vya polisi wa uhamiaji havitendi haki wala kulinda jamii, bali husababisha hofu na taharuki.

Video ya Mamdani, ambamo aliwataka viongozi wa Marekani kumchukua Mtume Muhammad (SAW) kama mfano katika sera zao za uhamiaji, ilisambaa kwa kasi kubwa katika mitandao ya kijamii na kuzua mijadala mikubwa.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii walieleza kuwa matumizi ya lugha hii ya kidini na kihistoria na Meya yanalenga kuvunja mitazamo potofu na kugusa dhamiri ya binadamu kupitia historia ya pamoja ya imani.

Habari inayohusiana:

Wachambuzi walibainisha kuwa hii ni mara ya kwanza katika historia ya New York kwa meya kunukuu Aya ya Qur’ani Tukufu na Hadithi ya Mtume Muhammad (SAW) hadharani mbele ya wakazi wa jiji, huku akirejea Hijra ya Mtume na misingi ya Kiislamu ya haki na huruma kwa wageni.

Baadhi ya wanablogu walielezea haiba ya Mamdani kuwa ya kuvutia, hasa katika kipindi hiki kinachoshuhudia kuongezeka wazi kwa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Walieleza kuwa si jambo rahisi kwa Mwislamu kufikia nafasi kama hiyo ya uongozi na kisha kujitambulisha wazi kwa kurejea marejeo yake ya Kiislamu.

Wengine waliona kuwa hotuba ya Mamdani inaweza kufungua mjadala mpana zaidi kuhusu sera za uhamiaji nchini Marekani, hasa katika jiji lenye tamaduni na dini nyingi kama New York.

Aidha, baadhi walithibitisha kuwa msimamo wake unaweza kuimarisha imani kati ya jamii ya Waislamu na mamlaka za mitaa, na kutoa ujumbe kuwa nafasi za kisiasa zinaweza kutekelezwa sambamba na utambulisho wa kidini na maadili ya kibinadamu—mfano adimu katika siasa za Marekani.

Tangu Januari 7, miji mbalimbali nchini Marekani imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa kupinga matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na ICE katika operesheni zake dhidi ya wahamiaji, operesheni zilizogharimu maisha ya raia wawili mjini Minneapolis.

Tangu kuapishwa kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, mnamo Januari 2025, maelfu ya maafisa wa serikali ya shirikisho—wengi wao wakiwa na silaha na wakijifunika nyuso—wamekuwa wakitekeleza misako katika miji ya Marekani kwa lengo la kuwakamata wahamiaji wasio na nyaraka halali.

3496336

captcha