IQNA

Gharama Nafuu ya Hija Ni Kipaumbele, Asema Rais wa Indonesia

11:45 - February 09, 2026
Habari ID: 3481911
IQNA – Uendelezaji wa Kijiji cha Hija cha Indonesia mjini Makkah ni mhimili mkuu wa ahadi ya Rais Prabowo Subianto ya kuhakikisha ibada ya Hija inakuwa nafuu zaidi, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa mamilioni ya Waislamu wa Indonesia.

“Kila mwenye kuhiji atapatiwa malazi yenye staha, msihofu. Ninaahidi huduma bora kabisa huko, kwani pia nimeazimia kupunguza gharama ya Hija kwa wananchi wa Indonesia,” alisema Rais wa Indonesia alipohutubia hafla ya maadhimisho ya miaka 100 ya Nahdlatul Ulama (NU) iliyofanyika Malang, Java ya Mashariki, siku ya Jumapili.

Akuhutubu mbele ya maulamaa na wafuasi wa NU, Rais Prabowo alieleza kuwa Indonesia imejaliwa neema ya kuwa na kiwanja chake binafsi cha ardhi kwa ajili ya maendeleo mjini Makkah, mji mtukufu zaidi kwa Waislamu.

Alisema Indonesia itaendeleza Kijiji cha Hija kwa ajili ya wanaotekeleza ibada za Hija na Umra, akiongeza kuwa mpango huo utahakikisha upatikanaji wa huduma bora na za gharama nafuu kwao.

Serikali pia itajitahidi kuhakikisha viwango vya juu kabisa vya huduma kwa mahujaji watakaokaa katika kituo hicho.

“Ndani ya miaka mitatu, tunatarajia Kijiji cha Hija chenye hadhi kukamilika. Katika miezi ijayo, tutakuwa na vyumba 1,000 kwa mahujaji wa Indonesia, kwani tumeazimia kujenga zaidi,” alibainisha Prabowo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Sekretarieti ya Taifa, Prasetyo Hadi, mwezi Januari Indonesia ilishinda zabuni ya kununua hoteli na ardhi mjini Makkah ambayo itaendelezwa kuwa Kijiji cha Hija cha Indonesia, makubaliano ya kihistoria yaliyochangiwa na mabadiliko ya sera za Saudi Arabia.

Hadi alieleza mafanikio hayo kuwa ni matokeo ya “diplomasia ya hali ya juu isiyo ya kawaida” ya Rais Prabowo, ambayo ilifungua fursa ya umiliki wa mali za kigeni mjini Makkah.

Habari inayohusiana:

Rosan Roeslani, Mkurugenzi Mtendaji wa Danantara Indonesia inayosimamia uwekezaji wa kimkakati wa serikali, pia alithibitisha ununuzi wa Hoteli ya Novotel Thakher Mecca pamoja na takribani hekta tano za ardhi kwa ajili ya kuanzisha Kijiji cha Hija cha Indonesia.

Hoteli hiyo ina vyumba 1,461 katika minara mitatu, na inaweza kuhudumia mahujaji 4,383 wa Indonesia, ikitoa malazi ya pamoja wakati wa msimu wa Hija kila mwaka.

Serikali inapanga kuongeza minara 13 zaidi, hivyo kuongeza jumla ya vyumba hadi 6,025, pamoja na huduma shirikishi zitakazoboresha faraja, ufanisi na huduma kwa mahujaji wa Indonesia, In shaa Allah.

3496341

Kishikizo: hija indonesia makka rais
captcha