
Sheikh al‑Naqshbandi alikuwa mtaalamu mahiri wa ibtihal (tenzi na dua za Kiislamu), na sauti yake iligeuka kuwa alama ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, hasa katika ibtihal zake zilizosikika kabla ya adhana ya Magharibi, zilizokuwa zinagusa nyoyo na kuwavutia mamilioni ya Waislamu.
Alizaliwa mwaka 1920 katika kijiji kimoja cha Mkoa wa Dakahlia nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka kumi, familia yake ilihamia mjini Tahta, Kusini mwa Misri, ambako alihifadhi Qur’ani Tukufu na kujifunza ibtihal kupitia vikao vya dhikri miongoni mwa wafuasi wa tariqa ya Kisufi ya Naqshbandiyya. Baba yake alikuwa kiongozi wa tariqa hiyo na mwanazuoni mashuhuri na ndio sababu akapata laqabu ya Naqshbandi.
Sheikh al‑Naqshbandi pia alikuwa mpenzi wa fasihi; alipenda kusoma maandishi ya Manfaluti, Abbas Mahmoud al‑Akkad na Taha Hussein, na alihifadhi mamia ya beti za mashairi ya Imam al‑Busiri, Ibn al‑Farid na Ahmad Shawqi.
Miongoni mwa taswira zilizoacha alama isiyofutika katika Ramadhani ya Misri ni sauti yake yenye nguvu, mvuto na upekee, iliyokuwa ikichochea hisia za watu wakati wa iftari. Ibtihal zake tamu, zilizotoka moyoni, ziligusa nafsi za Waislamu na kuwafanya warudie maneno yake kwa unyenyekevu na khushuu.
Al‑Naqshbandi alihesabiwa miongoni mwa nguzo kuu za dua, qiraa na qaswida, na alisifiwa kwa kuwa na uwezo wa kipekee katika munajaat na qasida, kiasi cha kutajwa kuwa mwanzilishi wa mkondo maalumu wa Ibtihal. Alijulikana kwa lakabu za "Sauti ya Wanyenyekevu," "Bulbul wa Mwenyezi Mungu" na “Imamu wa Waimbaji wa Kumsifu Mwenyezi Mungu.”
Hakukuwa na sherehe kamili katika enzi ya Rais wa zamani wa Misri Anwar Sadat bila ushiriki wa Sheikh al‑Naqshbandi. Inasimuliwa kuwa alikutana na mtunzi mashuhuri Baligh Hamdi na marehemu Wajdi al‑Hakim katika hafla ya uchumba wa mwana wa Sadat, ambapo rais aliwaambia waliokuwepo: “Washeni redio; nataka kumsikia Naqshbandi pamoja na Baligh Hamdi.”
Habari inayohusiana:
Baadaye, Sheikh al‑Naqshbandi alianza kurekodi ibtihal katika idhaa za Misri, ambazo zikawa sauti maarufu inayotangulia adhana ya Magharibi katika mwezi wa Ramadhani, zikijulikana kama waidhina wa nyoyo.
Sheikh Mohamed al‑Naqshbandi alifariki dunia mwaka 1976 akiwa na umri wa miaka 56, bila kuwa na maradhi yoyote yanayojulikana. Muda mfupi kabla ya kifo chake, aliandika wosia, akiomba azikwe karibu na mama yake katika makaburi ya Tariqa ya Khalwatiyya huko Al‑Bastain, na akaelekeza kuwa kusifanyike hafla za maombolezo bali rambirambi na taarifa za msiba zichapishwe tu kwenye magazeti.
Urithi wake wa kiroho na sauti yake bado unaendelea kuhuisha Mwezi wa Ramadhani, kuanzia Misri hadi Pwani ya Afrika Mashariki, ambako ibtihal na munajaat zake hupokelewa kwa heshima na mapenzi ya dhati.
4334443