IQNA

Ushiriki Mpana wa raia na wakazi katika Mashindano ya Qur’ani ya Qatar

14:03 - February 25, 2026
Habari ID: 3481991
IQNA – Mashindano ya Qur’ani Tukufu nchini Qatar yanaendelea kushuhudia ushiriki mkubwa wa raia na wakazi, wanaume na wanawake, katika mazingira yaliyojaa unyenyekevu na utukufu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Washiriki wanashindana katika kuhifadhi sehemu maalumu kutoka juzuu tano za mwisho za Qur’ani Tukufu, mashindano yanayosimamiwa na Wizara ya Wakfu na Mambo ya Kiislamu, ambayo imeandaa hafla hii katika hali ya kiroho na nidhamu ya hali ya juu.

Mitihani ya wanaume inafanyika katika Msikiti wa Imamu Muhammad bin Abdul Wahhab wakati wa jioni, kuanzia saa 9:30 alasiri (baada ya Swala ya Alasiri). Mitihani ya wakazi wa kiume ilianza tarehe 19 Februari na inatarajiwa kukamilika Jumatano ijayo.

Kwa upande mwingine, mitihani ya wasichana wakazi inaendelea kufanyika katika makao makuu ya Idara ya Da‘wah, chini ya usimamizi maalumu unaolenga faragha na heshima.

Vijana raia wa Qatar, wanaume na wanawake,  wanatarajiwa kushiriki katika mashindano haya tarehe 25 na 26 Februari 2026, kwa mujibu wa ratiba rasmi iliyoidhinishwa. Mpango huu unachukuliwa kuwa nguzo muhimu ya kielimu katika kukuza kizazi cha Qur’ani chenye uelewa, kinachojivunia utambulisho wake wa Kiislamu.

Kamati ya maandalizi imethibitisha kuwa maandalizi yote ya kiufundi na kiusafirishaji yamekamilika, huku mfumo wa kisasa wa kielektroniki wa upimaji ukitumika ili kuhakikisha usahihi, uwazi na uadilifu.

Majopo ya majaji yanaongozwa na vipaji mahiri vya vijana wa Kiqatar, huku kwa upande wa wanawake, kamati zikijumuisha majaji wanawake wa Kiqatar wenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi Qur’ani Tukufu. Hili linaonyesha nafasi ya mbele ya mashindano haya katika kuhudumia Kitabu cha Mwenyezi Mungu na watu wake katika Dola ya Qatar.

/3496550/

Habari zinazohusiana
Kishikizo: qurani tukufu qatar
captcha