Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne, Ali Akbar Pourjamshidian alieleza kuwa kamati maalum imeundwa nchini Iraq chini ya usimamizi wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, kwa ushirikiano wa karibu na maafisa wa Iran, ili kuhakikisha kuwa misafara ya mazishi na mapokezi rasmi nchini Iraq yanafanyika kwa kiwango cha juu kabisa cha heshima.
Bwana Pourjamshidian aliongeza kuwa katika ziara ya hivi karibuni nchini Iraq aliyoambatana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, mikutano ilifanyika na maafisa wakuu wa Iraq, wakiwemo Rais, Spika wa Bunge, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, na Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais. Katika mikutano hiyo, mipango kamili ya shughuli hizo ilikamilishwa.
Alisisitiza kuwa moja ya malengo makuu ya kuandaa hafla kubwa kama hiyo ni kuonyesha upya ahadi ya utiifu ya Umma wa Kiislamu kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Alibainisha kuwa matukio hayo nchini Iraq yatafanyika kwa kiwango cha kipekee na cha kimataifa, jambo linaloakisi mamlaka ya kidini ya Kiongozi huyo shahidi.
Kwa mujibu wa Pourjamshidian, uamuzi wa kufanya sehemu ya shughuli hizo nchini Iraq uliungwa mkono kwa nguvu na kamati ya maandalizi pamoja na familia ya Kiongozi huyo, kutokana na hadhi yake kuu ya kidini.
Alieleza kuwa wananchi wa Iraq, viongozi wa makabila, maafisa wa serikali, na wawakilishi wamesisitiza kuwa Kiongozi huyo shahidi alikuwa ni Marjaa wao (kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ambaye anafuatwa kwa mujibu wa hukumu za Kifiqhi anazotoa) na walitarajia hafla kama hizo zifanyike.
Aidha, alifafanua kuwa Kiongozi huyo shahidi alikuwa na shauku ya muda mrefu ya kuzuru makaburi matukufu ya Imam Ali (AS) na Imam Hussein (AS) katika uhai wake, lakini mazingira hayakuruhusu.
“Tunatumai kuwa kupitia mipango hii, mwili wake mtukufu utapelekwa kwa ajili ya ziara ya (ziyara). Kiongozi wetu shahidi yu hai mbele ya Mwenyezi Mungu, na kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, atatukuzwa kwa ziara ya maeneo hayo matakatifu,” aliongeza.
Maafisa wa Iraq walikuwa wametangaza hapo awali kuwa miji ya Najaf na Karbala imejitayarisha kikamilifu kuandaa shughuli hizo.
3498037