
Rais Pezeshkian amesema kuwa mashambulizi hayo yanapelekea kuongezeka hali ya kutokuwa na utulivu, kuzidisha gharama za kibinadamu na kiuchumi, pamoja na kochochea mvutano unaoendelea. Ameongeza kuwa njia ambayo utawala wa Marekani unafuata si ishara ya nguvu, bali ni kielelezo cha kuchanganyikiwa na kushindwa kupata suluhisho la kudumu.
Aidha, Rais Pezeshkian amesema kwamba Iran ilikuwa imechagua njia ya mazungumzo, ikafikia makubaliano na kutekeleza majukumu yake. Hata hivyo, Marekani ilijiondoa katika makubaliano hayo, kisha ikafanya mashambulizi mawili dhidi ya Iran katikati ya mazungumzo. Amesema kuwa hayo ni maamuzi yenye madhara makubwa yaliyofanywa na serikali ya Marekani kwa kutekeleza matamanio ya wavamizi wa kigeni.
Rais Pezeshkian pia amehoji: Je, si kweli kwamba Marekani imeingia kwenye uchokozi huu kama nguvu ya niaba ya Israel, kwa kuchochewa na utawala huo? Au je, si kweli kwamba sasa Israel imeamua kupigana na Iran hadi askari wa mwisho wa Marekani na hadi senti ya mwisho ya kodi ya mlipa kodi wa Marekani, huku gharama zikibebeshwa Iran, nchi za eneo hili, na hata Marekani yenyewe, ilhali Israel ikibaki salama? Je, kweli “Marekani Kwanza” bado ndio kipaumbele cha kwanza katika ajenda ya serikali ya Marekani leo?
Rais wa Iran pia amesisitiza kuwa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia yameonyesha wazi kuwa uwepo huo ni tishio. Amesema ni jambo linaloeleweka kwamba hakuna nchi itakayokubali kuacha kuimarisha uwezo wake wa kujilinda katika mazingira kama hayo. Kile ambacho Iran imefanya na inaendelea kufanya ni hatua za kujibu na kujilinda, si kuanzisha vita au uchokozi.
Vilevile, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa taifa la Iran halijawahi kuwa na uadui na mataifa mengine, ikiwemo watu wa Marekani, Ulaya na majirani wake. Ameongeza kuwa Wairani, hata walipokabiliwa na uvamizi au shinikizo kutoka nchi za kigeni katika historia yao, daima walitofautisha kati ya wananchi na tawala vamizi.
3496950/