
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, hafla hiyo ilifanyika katika makao makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Ulimwengu wa Kiislamu (ICESCO) mjini Rabat, na ilihudhuriwa na wanazuoni, mawaziri, mabalozi na wageni mashuhuri kutoka nchi mbalimbali.
Makumbusho hayo, ambayo ni miongoni mwa miradi ya kimataifa chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Kiislamu Duniani (Muslim World League), yanawakilisha mfano wa kisasa wa kuwasilisha Sira ya Mtume (SAW) kwa lugha ya wakati huu, kupitia ushirikiano wa kimkakati na ICESCO pamoja na Muungano wa Wanazuoni wa Kiislamu nchini Morocco.
Maonesho hayo yalifunguliwa mwaka 2022, na tangu wakati huo yamepokea mamilioni ya wageni kutoka kote ulimwenguni, kuanzia watu mashuhuri wa kimataifa hadi wananchi wa kawaida, hali inayoonyesha mafanikio yake katika kuvutia hadhira pana na kuimarisha ujumbe wake wa kielimu wa kimataifa.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu Duniani, Mohammed bin Abdul Karim Al-Issa, alisisitiza kuwa makumbusho hayo yanawakilisha hatua kubwa katika uwasilishaji wa Sira ya Mtume (SAW), kwa kubadilisha maandiko kuwa mandhari shirikishi kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Alieleza kuwa mbinu hiyo huwapa wageni uzoefu hai wa kielimu unaoongeza maarifa yao na kuimarisha uhusiano wao na Sira tukufu ya Mtume Muhammad (SAW).
Kwa mujibu wa maafisa, kufikiwa kwa idadi ya wageni milioni 10 kunaashiria mafanikio ya ushirikiano kati ya taasisi hizo tatu, ambapo mradi huo unaunganisha maadili ya kibinadamu na maudhui sahihi ya kielimu, huku ukiacha athari ya kina ya kihisia kwa wageni.
Hafla hiyo pia ilishuhudia uzinduzi wa sehemu mpya na kuongezwa kwa ensaiklopidia za kisasa za kielimu, ikiwemo jukwaa la “Mo’een” linalotumia akili mnemba (AI), pamoja na mabanda shirikishi yanayoonesha kwa kina vipengele vya maisha ya Mtume (SAW) ikiwemo maisha yake ya kila siku, Hijra, na vitu vyake binafsi, yote yakioneshwa kwa mtindo wa kisasa unaochanganya uhalisia na ubunifu.
Baada ya hafla hiyo, kulifanyika kikao cha majadiliano ya kisayansi kilichowahusisha wanazuoni na wataalamu kutoka nchi mbalimbali, ambapo walijadili vipengele vya kielimu na kiakili vya makumbusho hayo pamoja na nafasi yake katika kuongeza uelewa wa Sira ya Mtume (SAW) na uhusiano wake na changamoto za kisasa, jambo linaloimarisha nafasi yake kama jukwaa la kimataifa la majadiliano ya kielimu.
/3497253