
Mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Indonesia, Pakistan, Misri, Jordan, Falme za Kiarabu (UAE), Qatar na Uturuki wamelaani hatua hiyo ya jinai.
Walowezi hao waliinua bendera za Israel katika ngazi zinazoelekea kwenye Qubbat As‑Sakhra, wakapiga nara na kuimba wimbo wa taifa wa Israel chini ya ulinzi wa polisi. Waliingia katika eneo la msikiti kupitia Lango la Al‑Maghariba, ambalo liko chini ya udhibiti wa mamlaka za Israel.
Mawaziri hao wamesema wanakataa jaribio lolote la kubadilisha sura ya kihistoria, kisheria na ya kidemografia ya Al‑Quds ya Mashariki iliyo chini ya ukaliaji, au kitendo chochote kinachotishia utakatifu wa maeneo yake ya Kiislamu na Kikristo.
Msikiti wa Al‑Aqsa, ambao ni miongoni mwa maeneo matakatifu matatu makuu katika Uislamu, umekuwa ukishuhudia mara kwa mara mivutano na makabiliano, ikiwemo uvamizi wa walowezi na vikwazo kwa waumini Waislamu wanaotaka kuswali, tangu Al‑Quds ya Mashariki ilipokaliwa mwezi Juni mwaka 1967.
Eneo la Msikiti wa Al‑Aqsa linasimamiwa na Wizara ya Awqaf ya Jordan, ambayo kisheria ina mamlaka ya kusimamia eneo hilo na kudhibiti upatikanaji wake.
Walowezi wa Israel, wanaoliita eneo hilo “Temple Mount”, wanajaribu kuanzisha uwepo wa kudumu ndani ya eneo hilo ili kufanya ibada za Kiyahudi katika nyakati fulani. Baadhi ya wabunge waandamizi wa Israel, akiwemo waziri wa eti usalama ambaye ni mfuasi wa mrengo mkali wa kulia Itamar Ben‑Gvir, wameunga mkono waziwazi mipango hiyo.
/3497697