IQNA

‘Kila Hatua Tunayochukua ya Kukataa Uvamizi ni Ushindi’: Katibu Mkuu wa Hizbullah

22:47 - June 20, 2026
Habari ID: 3482382
IQNA – Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa utawala wa Kizayuni umefeli katika njama zake zote za kutaka kuangamiza harakati hiyo ya mapambano (Muqawama).

Sheikh Naim Qassim ametoa kauli hiyo yenye kujaa imani na yakini, akisisitiza kuwa Israel itafurushwa kutoka katika ardhi ya Lebanon, kwani mpango wa utawala huo wa kutaka kuiondoa harakati ya mapambano umegonga mwamba.

Akihutubia katika hafla ya Baraza Kuu la Ashura mjini Beirut siku ya Ijumaa, Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassim, alieleza bayana kuwa “adui ameshindwa kuvunja imani yetu, msimamo wetu thabiti, ustahimilivu wetu, na uwepo wetu endelevu katika uwanja wa mapambano, na sisi tunavumilia kila aina ya dhiki na vikwazo.”

Alisema kuwa kanuni zinazoiongoza harakati hiyo ya mapambano “ni miongoni mwa thamani tukufu zaidi duniani.”

“Hatuhofii mauti, na hili ni nguzo muhimu ya ushindi,” alisisitiza Sheikh Qassem, huku akiongeza: “Wakati adui anapotukabili kwa silaha, sisi tunamkabili kwa silaha vilevile.”

Sheikh Qassim alifafanua kuwa mapambano yenyewe ni aina ya ushindi, akisisitiza kuwa “kila hatua tunayochukua ya kukataa uvamizi ni ushindi tosha.”

“Hata kama hatutabaki hata mmoja wetu, kwa kisingizio kuwa kuna tishio la mauti, kwetu sisi, tunatekeleza wajibu wetu wa kidini na kimaadili, na kwa sababu hiyo, hatuogopi kufa.”

Sheikh Qassim alibainisha zaidi kuwa Hizbullah inabaki imejitolea kikamilifu katika misingi ya Muqawama na ukombozi wa ardhi za Lebanon zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni. Alisisitiza kuwa harakati hiyo imekuwa ikifanya kazi ndani ya mfumo wa katiba ya Lebanon na Mkataba wa Taif wa 1989, ambao ulihitimisha miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Kiongozi huyo wa Hizbullah aliongeza kuwa njama za Israel za kutaka kuiondoa Muqawama zimefeli, na kwamba vikosi vya utawala huo hatimaye vitafurushwa kutoka ardhi yote ya Lebanon na wananchi wa Lebanon wenyewe.

“Tulizaliwa tukiwa huru, na tumechagua kukataa dhulma,” aliongeza.

Sheikh Qassim alisisitiza tena kwamba “kupata hasara kubwa ni afadhali kuliko kujisalimisha na kushindwa.”

Alionya kuwa Lebanon inapitia “kipindi hatari zaidi,” akibainisha kuwa mpango wa adui ni kuangamiza Muqawama na watu wake, na kufuta kabisa uwepo wake nchini Lebanon. “Hili ni tishio kubwa zaidi kwa mustakabali wa nchi yetu,” alionya.

Alieleza kuwa adui alijaribu kufunga vivuko vya anga, baharini, na nchi kavu ili kuzuia kuingia kwa silaha, teknolojia, na kila kitu kinachoweza kuimarisha Muqawama, na pia kuzuia ujenzi ili wananchi waendelee kuwa wakimbizi na wasio na makazi.

Aidha, alisisitiza kuwa adui alijaribu kuchochea uhasama kati ya Jeshi la Lebanon na Muqawama, lakini busara ya Jeshi ilifeli njama hiyo.

Kuelekea mwisho wa hotuba yake, alitoa wito kwa wananchi wa Lebanon “kuzingatia wajibu wao wa kidini; kwani kuhusiana na ushindi, hilo liko mikononi mwa Allah (SWT).”

3497900/

Habari zinazohusiana
captcha