IQNA

Sheikh Naim Qassim ateuliwa kuongoza harakati ya Hizbullah ya Lebanon

16:16 - October 29, 2024
Habari ID: 3479668
IQNA-Sheikh Naim Qassim aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Mpya wa harakati hiyo ya mapambano baada ya mtangulizi wake Sayyid Hassan Nasrullah kuuawa shahidi katika hujuma ya Israel kusini mwa Beirut, mwezi uliopita.

Baraza la Ushauri la Hizbullah ambacho ni chombo kikuu cha maamuzi cha harakati hiyo leo Jumanne limemteuwa Sheikh Qassim aliye na umri wa miaka 60 kushika wadhifa huo kufuatia kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrallah. 

Baraza la Ushauri la Hizbullah limemteuwa Sheikh Naim Qassim kuwa Katibu Mkuu wa harakati hiyo na kumkabidhi bendera kwa baraka zote katika safari yake mpya akiwa Katibu Mkuu wa harakati hiyo ya Muqawama. Limesema linamuomba Mwenyezi Mungu ampe mafanikio katika wadhifa wake adhimu wa kuingoza Hizbullah na mapambano yake ya Kiislamu. 

Taarifa ya Baraza la Ushauri la harakati ya Hizbullah pia imewaahidi wahanga waliouawa shahidi, wanamuqawama wa Kiislamu pamoja na taifa imara  la Lebanon kwamba Hizbullah itasimamia misingi,  kanuni, malengo na njia zake ili kuendeleza  mapambano ya ukombozi hadi ushindi utakapopatikana. 

Sheikh Qassim ni shakhsia mkongwe wa harakati ya Muqawama ya Hizbullah na amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa harakati hiyo tangu mwaka 1991. 

3490481

 

Habari zinazohusiana
captcha