IQNA

Msimamo wa Imam Hussein (AS) ni kielelezo cha kupinga dhulma ya zama hizi

19:29 - July 06, 2025
Habari ID: 3480908
IQNA – Mwanazuoni mmoja kutoka Iran amesema kuwa mwamko wa Imam Hussein (AS) dhidi ya Yazid bin Muawiya unabaki kuwa mfano wa milele wa kupambana na dhulma za zama hizi na uonevu wa kimataifa.

Katika semina ya mtandaoni iliyoitwa “Uongozi Qur’ani na Mwamko wa Imam Hussein (AS)” iliyofanyika Jumamosi, Hujjat-ul-Islam Najaf Lakzaei, Rais wa Chuo cha Sayansi na Utamaduni wa Kiislamu na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Baqir al-Olum, alisema kuwa Imam Hussein (AS) alitazama utawala wa Yazid kama haramu na wa kidhalimu, akifananisha na utawala wa Firauni huko Misri ya kale.

"Utawala wa Yazid ulikuwa wa udikteta na ubaguzi, ina ulitishia ustawi wa Uislamu," alisema Lakzaei. _"Imam Hussein (AS) alisimama kuwakomboa watu kutokana na mfumo huo dhalimu."

Aliashiria riwaya ya Imam Hussein (AS) inayosisitiza wajibu wa “kuamrisha mema na kukataza maovu”, alibainisha kuwa uongozi wa Kiislamu wakati huo ulikuwa mikononi mwa wasiofaa. "Ndiyo maana Imam aliona ni wajibu wa kidini kupinga dhulma," Lakzaei alisema.

Akirejea safari ya Imam Hussein (AS) kutoka Madina, Lakzaei alieleza kuwa Imam alikataa kutoa utii kwa Yazid licha ya shinikizo kutoka kwa mtawala wa mji, kisha akaondoka baada ya kusoma aya ya 21 ya Surah Al-Qasas: “Akasema: 'Mola wangu! Niokoe kutoka kwa watu madhalimu.’”

Kulingana na Lakzaei, aya hiyo inayoonyesha alivyookolewa Nabii Musa kutoka kwa Firauni, inaonesha jinsi Imam Hussein (AS) alivyofananisha utawala wa Yazid na wa Firauni.

Lakzaei aliongeza: “Imam Hussein aliona hali yake kuwa sawa na ile ya Musa, ya kupambana na dhalimu, sambamba na kutetea haki na kuilinda dini.” Aliongeza kuwa Yazid, kupitia mashairi yake, alidhihaki Wahyi na kuiona dini kama mchezo wa kisiasa wa ukoo wa Bani Hashim.

"Ili kufahamu vizuri mwamko wa Imam Hussein (AS), ni lazima tusome hadithi za Musa na Firauni katika Surah Al-Qasas, Taha, Al-Baqarah, na Al-A’raf,"_alisema Lakzaei.

Akilinganisha simulizi ya sura hiyo ya Qur’ani na Karbala, Lakzaei alieleza: “Kama Firauni na wafuasi wake walivyoshindwa, Yazid na walioambatana naye pia walishindwa. Ingawa Imam Hussein na maswahaba wake walikufa shahidi, utawala wa Yazid haukuweza kudumu.”

Aliwalaani watu kama Umar ibn Sa’d, Ubayd Allah ibn Ziyad na Shimr waliompinga Imam Hussein (AS) kwa maslahi ya dunia, lakini wakabaki katika fedheha ya dunia na Akhera.

"Imam Hussein (AS) alikuwa sauti ya haki, kama ambavyo katika zama hizi Imam Khomeini alipambana  na dhulma ya kimataifa," alihitimisha Lakzaei.

"Leo, ni juu yetu kuendeleza njia ya Imam Hussein (AS) kwa kupinga dhulma na mfumo wa ubeberu wa kimataifa. Kama tungekuwepo wakati wa Imam Hussein (AS), tungechagua upande upi wa haki au wa batili? Chaguo hilo bado ni muhimu hadi leo."

3493725

captcha