IQNA

Maafisa wasema Iraq iko tayari kwa matembezi ya Arbaeen

19:26 - August 04, 2025
Habari ID: 3481038
IQNA – Mamlaka za Iraq zimezindua maandalizi makubwa ya huduma na usalama, huku mamilioni ya wafanyaziara wakitarajiwa kuelekea Karbala kwa ajili ya matembezi ya Arbaeen.

Mafisa wasema Iraq iko tayari kwa matembezi ya Arbaeen

IQNA – Mamlaka za Iraq zimezindua maandalizi makubwa ya huduma na usalama, huku mamilioni ya wafanyaziara wakitarajiwa kuelekea Karbala kwa ajili ya matembezi ya Arbaeen.

Arbaeen ni mojawapo ya mikusanyiko mikubwa kabisa ya kidini duniani, ikikumbusha siku ya arobaini baada ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), katika karne mwaka 61 Hijria Qamaria.. Tukio hili hufanyika Karbala, Iraq, na huvutia makumi ya mamilioni ya wafanyaziara kila mwaka, wengi wao wakiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia kutoka Iraq na mataifa mbalimbali duniani.

“Umeme wa kutegemewa, huduma muhimu, na usalama wa barabara kuu ni miongoni mwa vipaumbele vikuu,” alisema Ahmed Mousa al-Abadi, msemaji wa Wizara ya Umeme ya Iraq, kwa mujibu wa Middle East News.

Al-Abadi alieleza kuwa wizara yake imeanzisha mpango wa dharura unaolenga kuboresha hali ya umeme katika Karbala na kando ya njia za hija.

Hatua hizo ni pamoja na kurekebisha mtandao wa usambazaji umeme, kufunga transfoma mpya, na kufanya matengenezo kwenye miundombinu ya umeme iliyopo. Lengo ni kupunguza mzigo kwenye mfumo hasa katika maeneo yenye msongamano kama vile sehemu za malazi, vituo vya matibabu, na mahema ya muda ya kutoa huduma (mawkib) yanayosimamiwa na waumini wa kujitolea.

Wakati huo huo, serikali ya Karbala kwa kushirikiana na kamandi ya operesheni za usalama kitaifa, wizara kadhaa, na wasimamizi wa Haram takatifu za Imam Hussein (AS) na Hadhrat Abbas (AS), wanaweka mikakati ya kina ya usalama na huduma za vifaa.

Majimbo jirani ya Najaf, Wasit, Erbil, Kirkuk, na Muthanna yamepeleka pia vifaa na watumishi kusaidia Karbala kukabiliana na mahitaji ya watu na changamoto za kiutawala.

Maafisa wanakadiria kwamba zaidi ya mahujaji milioni 20 huenda wakahudhuria kumbukumbu ya mwaka huu – hali inayotaka uratibu wa hali ya juu katika miundombinu, huduma za umma, na usalama wa wananchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iraq, Abdul Amir al-Shammari, ambaye pia ni mkuu wa Kamati Kuu ya Usalama kwa Hijja Kubwa, ameagiza ukaguzi wa mwisho wa hatua zote za maandalizi.

Amesema wizara yake imetumia uwezo wake wote kuhakikisha usalama wa wafanyaziyara, ikiwemo usakinishaji wa kamera za ulinzi na kuimarisha ulinzi katika njia kuu na maeneo ya mikusanyiko.

“Nimewaagiza manaibu, makamanda na viongozi wote wawepo kimwili katika maeneo ya utekelezaji na wasimamie kwa karibu nyanja zote za usalama,” alisema al-Shammari.

Akizungumzia ujio wa mamilioni ya wafanyaziyara kutoka Iraq na mataifa ya nje, alisisitiza kuwa mafanikio ya mpango wa usalama yanategemea “usahihi na upangaji wa nguvu kazi kwa weledi.”

3494119

Kishikizo: iraq arbaeen
captcha