Akizungumza Ijumaa mjini Beirut katika kikao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, Sheikh Darian alisisitiza kuwa ajenda ya pamoja ya wananchi wote wa Lebanon, wakiwemo Waislamu, ni kulinda maslahi ya taifa. Aliongeza kuwa, ili kukabiliana na changamoto na vitisho vinavyoikabili Lebanon, wananchi wote wanapaswa kusimama pamoja kwa umoja.
Kwa upande wake, Araghchi alisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inathamini jumuiya zote za kidini nchini Lebanon. Alibainisha kuwa umoja wa Walebanon wote ni muhimu katika kulinda uhuru na mamlaka ya nchi, hasa ikizingatiwa sera za kichokozi za utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon.
Mwanadiplomasia huyo wa juu wa Iran alisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za kuleta ukaribu kati ya madhehebu ya Kiislamu, na akasema Iran iko tayari kuimarisha ushirikiano na mataifa yote ya Kiislamu katika mwelekeo huo.
Aidha, aliongeza kuwa Iran imejidhatiti kupanua uhusiano wake na Lebanon katika nyanja zote zenye maslahi ya pamoja.
Araghchi aliwasili Beirut Alhamisi kwa mazungumzo na viongozi wa juu wa Lebanon kuhusu uhusiano wa pande mbili na mwelekeo wa matukio ya kikanda.
/3496025