IQNA

Kikao cha Qur’ani mjini Najaf chaadhimisha Maulidi ya Imam Zaman

8:12 - February 07, 2026
Habari ID: 3481896
IQNA – Baraza la Kisayansi la Qur’ani Tukufu chini ya Idara ya Usimamizi wa Haram Takatifu ya Hadhrat Abbas (AS) liliandaa kikao maalumu cha Qur’ani mjini Najaf kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa Imam Zaman (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake kwa heri).

Mkusanyiko huo wa Qur’ani wa katikati ya Shaaban (Nisfu Shaaban) ulifanyika katika muktadha wa mpango maalumu wa Qur’ani kwa wanafunzi wa Hauza (Chuo cha Kiislamu) cha Najaf, kwa mujibu wa taarifa ya Al-Kafeel.

Hafla hiyo ilianza kwa kisomo cha aya tukufu za Qur’ani kutoka kwa Sheikh Ahmed al-Falih, kikifuatiwa na mhadhara wa Qur’ani uliotolewa na Ammar al-Husseini, na kisha Sheikh Muhammad al-Asadi akafanya kisomo cha pili.

Sheikh Wissam al-Sabti, mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Qur’ani katika Hauza ya Najaf, alisema kikao hicho kilifanyika katika shule ya Khatam al-Anbiya (SAW) kwa ushiriki wa kundi la wanafunzi wa elimu ya dini. Alieleza kuwa tukio hilo ni sehemu ya jitihada endelevu za kueneza utamaduni wa Qur’ani miongoni mwa tabaka mbalimbali za jamii katika majimbo yote ya Iraq, hususan miongoni mwa wanafunzi wa Hauza ya Najaf.

Aliongeza kuwa vikao kama hivyo vya Qur’ani huandaliwa kwa lengo la kuwaongoza wanafunzi na kusisitiza umuhimu wa kusoma na kutafakari Qur’ani Tukufu, kupitia programu na shughuli zinazofanyika karibu na maeneo wanayoishi wanafunzi.

Sheikh al-Sabti alibainisha kuwa mpango huu wa Qur’ani unajumuisha mafundisho ya misingi ya elimu ya Qur’ani, maandalizi ya wasomaji (qurra), na kuendeleza ujuzi wa kisomo cha Qur’ani, sambamba na programu maalumu ya kuwaandaa kundi teule la wamisionari kupitia kozi za kitaalamu.

Mkusanyiko huo ulifungwa kwa qasida na dua zilizoelezea maisha na wasifu wa Imam Mahdi (AS), zilizotolewa na Sheikh Ali Zarkani.

Habari inayohusiana:

Sikukuu ya Nisfu Shaaban, inayoadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Imam Zaman (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), huadhimishwa tarehe 15 ya mwezi wa Shaaban kwa kalenda ya Hijria.

Mwaka huu, Waislamu wa Kishia kote ulimwenguni waliadhimisha tukio hili tukufu siku ya Jumatano, Februari 4.

.Quranic Session in Najaf Marks Imam Zaman Birthday

Quranic Session in Najaf Marks Imam Zaman Birthday

Quranic Session in Najaf Marks Imam Zaman Birthday

4332602

 
 
Kishikizo: najaf imam mahdi shaaban
captcha