
Hassan Rashid Jawad al-Abaiji alitoa kauli hiyo katika hafla ya ufunguzi wa mkutano wa nne wa kimataifa wa kisayansi wa “Irshad”, uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Warith al-Anbia mjini Karbala, Iraq.
“Malezi ya haiba ya Kiislamu kwa misingi ya Qur’ani, Sunna ya Mtume (SAW) na mwenendo wa Ahl al-Bayt (AS), pamoja na kuimarisha tunu za Tauhidi, ndizo nguzo za kuunda jamii kamilifu na yenye maadili,” alieleza.
Aliongeza kuwa vyanzo vya sheria ya Kiislamu vimejengwa juu ya mihimili miwili mikuu: Qur’ani Tukufu na Sunna ya Mtume (SAW), sambamba na hotuba na nasaha za Ahl al-Bayt (AS) kama zilivyopokewa katika Nahj al-Balaghah, Sahifah Sajjadiyah na Risalat al-Huqquq.
“Qur’ani iko mstari wa mbele miongoni mwa vyanzo hivi, kwa kuwa ni Neno hai linalofaa kwa kila zama na kila mahali,” alisisitiza.
Al-Abaiji alibainisha kuwa mawaidha ya Mtume Mtukufu (SAW) yanatoa mfumo mpana wa malezi unaogusa nyanja zote za maisha ya mwanadamu, za kimada na kiroho, kielimu, kimaadili na kijamii. Alieleza kuwa Mtume (SAW) alikuwa ni kielelezo na mwalimu wa kwanza wa Umma, na kiongozi wa mchakato wa malezi na mwongozo katika vipengele vyake vyote vya kisaikolojia, kijamii na kimaadili.
Kwa mujibu wake, tafiti za kisasa zimeonesha kuwa mbinu ya Mtume (SAW) inajumuisha maelekezo ya vitendo yanayomwezesha mwanadamu kukabiliana na changamoto za maisha, kusahihisha mwenendo, na kukuza stadi za kiakili, kisaikolojia na kijamii. Mbinu hiyo, alisema, ni halali na yenye uhalisia kwa kila zama na mahali, na hotuba yake tukufu huchangia kujenga haiba yenye afya na mizani, na kuikomboa jamii kutokana na kurudi nyuma na ukoloni wa kitamaduni.
Al-Abaiji alisisitiza kuwa utekelezaji wa mafundisho haya katika mchakato wa elimu, mitaala ya shule na taasisi za malezi utafungua upeo mpya wa kutekeleza nadharia ya elimu ya Kiislamu, na kuandaa kizazi chenye imani, mizani na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kisasa, huku kikijenga jamii yenye fadhila inayozingatia uwiano wa mahitaji ya kimada na ya kiroho ya mwanadamu.
Habari inayohusiana:
Awamu ya nne ya mkutano wa kimataifa wa “Irshad” ilifanyika chini ya kaulimbiu: “Miongozo ya kuchunguza matatizo ya wanawake Waislamu katika kivuli cha changamoto za uvamizi wa kitamaduni”, likiwa ni sehemu ya programu za Taasisi ya Kusimamia Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS), iliyoko Karbala, Iraq, za kuimarisha misingi ya kidini na kuasisi maadili yanayotokana na Qur’ani na mwenendo wa Ahl al-Bayt (AS).
4334228