
Hatua ya fainali ya mashindano hayo imeandaliwa na Jumuiya ya Kisayansi ya Qur'ani Tukufu, inayohusiana na Idara ya Usimamizi wa Haram Tukufu ya Hadhrat Abbas (AS).
Kwa mujibu wa tovuti ya Al‑Kafeel, wasomaji wa Qur'ani kutoka zaidi ya nchi 20 za Kiarabu na zisizo za Kiarabu wanashiriki katika shindano hili, jambo linaloonesha upeo wake wa kimataifa katika ulimwengu wa Qur'ani.
Mashindano hayo yanasimamiwa na kamati ya kimataifa ya maqurra, wakiwemo Sheikh Muhammad Bassiouni kutoka Misri, Bassem Al‑Abidi na Mushtaq Al‑Ali kutoka Iraq, Sheikh Muhammad Asfour kutoka Misri, Sayed Hassanein Al‑Helou kutoka Iraq, pamoja na Seyed Karim Mousavi kutoka Iran.
Katika kipindi cha nane cha mashindano, Qari Maman Sitawaan kutoka Indonesia na Qari Jawad Hassani kutoka Afghanistan walishiriki katika kundi la watu wazima. Baada ya tathmini, qari kutoka Afghanistan alifanikiwa kufuzu kwenda hatua inayofuata. Katika kundi la vijana, Qari Mohammad Ali Sadiq kutoka Iraq alitinga raundi ijayo.
Kipindi hicho pia kilijumuisha hotuba ya Reza Al‑Raz, mwandishi na mwongozaji wa sanaa kutoka Lebanon. Alitambulisha Qur'ani Tukufu kama chanzo kikuu cha msukumo wa kazi zake za kisanii, akibainisha kuwa kazi yake ya hivi karibuni ni tamthilia ya watoto inayokuza maadili ya Qur'ani na kuwahimiza watoto kujifunza, kusoma na kuhifadhi Kitabu Kitukufu.
Al‑Raz alisisitiza kuwa uhusiano na Qur'ani haupaswi kuwa wa sauti pekee, bali ujengwe juu ya tafakkur, uelewa na kuifanya Qur'ani kuwa mtindo wa maisha.
Zaidi ya mwaka mmoja uliopita, alipoteza uwezo wa kuona na mkono wake wa kushoto kufuatia milipuko ya kile kilichojulikana kama “pager explosions” nchini Lebanon. Hata hivyo, akiongozwa na subira na ustahimilivu wa Hadhrat Abbas (AS), ameendelea na shughuli zake za Qur'ani na sanaa kwa kutegemea teknolojia za kisasa kama akili bandia (AI) na usomaji wa kielektroniki.
Mashindano ya usomaji wa Qur'ani ya Al‑Ameed hufanyika kila mwaka kama moja ya juhudi za Ataba ya Hadhrat Abbas (AS), yakilenga kusambaza utamaduni wa Qur'ani Tukufu na kuimarisha nafasi ya Qur'ani kama mwongozo thabiti wa maisha ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla.
3496576