
Mwanamke pekee Mwislamu aliyekuwa katika Tume ya Uhuru wa Kidini ya Ikulu ya White House amejiuzulu wadhifa wake.
Sameerah Munshi, aliyeteuliwa na Trump mwaka 2025, alitangaza kujiuzulu kwake akieleza kuwa hatua hiyo imetokana na “dhuluma na ukatili” unaofanywa na utawala wa Trump ndani ya nchi na katika uwanja wa kimataifa.
Alisema kuwa uamuzi wake pia ni ishara ya kupinga kuondolewa kwa Kamishna Carrie Prejean Boller, ambaye aliondolewa katika wadhifa wake mwezi uliopita baada ya kutumia kikao cha kusikiliza maoni kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi (antisemitism) kueleza ukosoaji wake kuhusu Israel na Uzayuni.
“Katika nchi hii, watu wa dini wanaondolewa haki yao ya kujieleza kwa uhuru, na hata maisha yao yanawekwa hatarini kwa sababu ya misimamo yao ya dhati kuhusu Palestina, yote haya kwa ajili ya ajenda ya kisiasa ya Uzayuni,” Munshi aliandika katika barua yake ya kujiuzulu iliyochapishwa kwenye Substack.
“Kuondolewa kwa kamishna Mkatoliki kwa sababu ya kutoa maoni ya upinzani yanayotokana na imani yake ni kinyume kabisa na uhuru wa kujieleza na uhuru wa dini ambao nilikuwa nikitetea.”
Katika barua yake, Munshi alieleza kuwa kujiuzulu kwake kunakwenda sambamba na kuondolewa rasmi kwa mjumbe wa tume hiyo, Carrie Prejean Boller, kutoka katika bodi na Rais Trump.
Boller, ambaye ni mshindi wa zamani wa shindano la Miss California USA, alifukuzwa kutoka kwenye tume hiyo mwezi Februari. Dan Patrick, Naibu Gavana wa Texas na mwenyekiti wa tume hiyo, alisema kuwa Boller alijaribu “kupotosha mwelekeo wa kikao” ambacho kilikusudiwa kujadili suala la chuki dhidi ya Wayahudi. Alishutumiwa pia kwa kusukuma mbele “ajenda binafsi na ya kisiasa.”
Munshi pia alionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu vita ambayo serikali ya Marekani imeanzisha dhidi ya Iran, akisema kuwa vita hivyo vilianza bila idhini inayotakiwa kwa mujibu wa Katiba ya Marekani au kibali cha Bunge.
“Mimi ni Sameerah Munshi. Nimechaguliwa na Rais na ninahudumu kama mshauri wa Tume ya Uhuru wa Kidini ya White House. Leo ninajiuzulu kutokana na dhuluma na ukatili wa utawala huu ndani ya nchi na nje ya nchi,” ilisema taarifa yake.
Munshi alikosoa vikali hatua za utawala wa Trump nchini Iran, na kusema kuwa serikali inawajibika kwa vifo vya raia, wakiwemo watoto, vilivyosababishwa na operesheni za kijeshi. Aidha, amesema kuwa hatua hizo zinafanywa ili kuimarisha Israel, ambayo aliitaja kuwa ni “dola inayotekeleza mauaji ya halaiki.”
“Sijiuzulu kwa sababu ya hofu au vitisho kutoka kwa yeyote aliyehusiana na tume hii, serikali, au kundi lolote la maslahi. Najiuzulu kwa sababu nimeshuhudia kwa macho yangu dhuluma zinazofanywa na baadhi ya wanachama wa tume hii, na sitaki tena kuhusishwa nazo,” aliandika.
/3496764/