
Makumi ya maelfu ya raia wa Iraq walikusanyika katika miji mikubwa kuadhimisha ushindi huo wa Iran, saa chache baada ya Marekani kukubali masharti ya Iran kuhusu usitishaji wa mapigano.
Mkusanyiko mkubwa zaidi ulifanyika siku ya Jumatano katika Uwanja wa al‑Tahrir mjini Baghdad, ambapo waandamanaji walionesha uungaji mkono wao kwa Mhimili wa Muqawama (Mapambano ya Kiislamu) na kutaja makubaliano hayo kuwa ushindi kwa kambi yao.
Umati wa watu ulipeperusha bendera za Iran, Hizbullah na makundi mengine ya muqawama, huku pia wakibeba picha za Ayatollah Sayyid Ali Khamenei, kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyeuawa shahidi siku 40 zilizopita, pamoja na Sayyid Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hizbullah ambaye pia aliuawa shahidi, sambamba na picha za viongozi wengine waliouawa katika mapambano hayo.
Shangwe hizo zilifuatia tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump, aliyethibitisha kuwa Marekani imekubali masharti ya vipengele kumi ya Iran kuhusu usitishaji wa mapigano.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema masuala mengi yaliyokuwa yakisababisha mvutano kati ya Marekani na Iran yalikuwa yamepata suluhu, na kwamba kipindi cha wiki mbili cha kusitisha mapigano kitatoa nafasi ya kuendelea na mazungumzo.
Makubaliano hayo yanatajwa kuwa hatua muhimu katika vita vilivyoanza tarehe 28 Februari, wakati Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa kuwaua maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa Iran, akiwemo Imam Khamenei.
Baada ya tangazo la kusitisha mapigano, Muqawama wa Kiislamu nchini Iraq ulisema utasimamisha mashambulizi dhidi ya malengo ya Marekani na Israel kwa muda wa wiki mbili.
Juhudi za makundi ya muqawama wa Iraq katika vita vilivyodumu siku 41 zimetajwa na wengi kuwa ushahidi wa uhusiano wa karibu na mshikamano uliopo kati ya watu wa Iraq na Iran.
Wakati maadui walipolenga kudhoofisha mamlaka ya Iran na kuvuruga utulivu wa eneo la Asia Magharibi, makundi ya muqawama ya Iraq yaliungana na Jamhuri ya Kiislamu kwa mshikamano, yakitekeleza mashambulizi ya kulenga vituo vya kijeshi vya Marekani na malengo yanayohusishwa na Israel ndani ya Iraq na maeneo mengine.
Hatua hizo ni utetezi wa haki ya Iran kujilinda pamoja na kupinga ushawishi wa nguvu za kigeni ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikihusishwa na siasa za eneo hilo.
Katika kipindi chote cha vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja, wananchi wa Iraq, kama ndugu zao wa Iran, waliendelea kuonesha msimamo wao kwa mapambano ya haki na uadilifu. Wapiganaji wa makundi mbalimbali ya muqawama waliripotiwa kusababisha hasara kubwa kwa upande wa adui.
Msaada kwa Iran katika kipindi hicho pia uliibua maandamano makubwa nchini Iraq, ambapo maelfu ya watu walijitokeza kuonesha mshikamano wao, hususan katika mkutano mkubwa uliofanyika Baghdad.
3497019