
Msemaji wa jeshi la Yemen, Jenerali Yahya Saree, amesema kuwa uchokozi wa kikatili unatekelezwa na tawala hasimu za Marekani na Israel, ambazo zinalenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mhimili wa Jihad na Muqawama , pamoja na umma mzima wa Kiislamu, kwa lengo la kuanzisha “Israel Kubwa,” chini ya kivuli cha mpango wa “kubadilisha Mashariki ya Kati.”
Amesema kuwa ni muhimu kwa Marekani na Israel kujibu mara moja juhudi za kidiplomasia za kimataifa zinazolenga kusitisha vita dhidi ya Iran na nchi za mhimili wa Muqawama. Ameongeza kuwa vita dhidi ya Iran ni vya kidhalimu na vinahatarisha utulivu na usalama wa kikanda na kimataifa pamoja na kudhuru uchumi wa dunia.
Jenerali Saree amebainisha kuwa jeshi la Yemen liko tayari kwa uingiliaji wa moja kwa moja wa kijeshi endapo muungano wowote mpya utaundwa pamoja na Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mhimili wa Jihad na Muqawama.
Aidha amesema jeshi la Yemen halitaruhusu Bahari Nyekundu kutumiwa kutekeleza operesheni za uhasama za Marekani na Israel dhidi ya Iran au dhidi ya nchi yoyote ya Kiislamu.
Msemaji huyo wa jeshi la Yemen ameongeza kuwa operesheni zao za kijeshi zinalenga tu maadui wawili ambao ni utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani kwa lengo la kuzuia mpango wa Kizayuni, na hazilengi watu wa mataifa ya Kiislamu.
Jenerali Saree pia amesisitiza umuhimu wa kutekelezwa kwa makubaliano ya Gaza na kutimizwa kwa wajibu uliomo ndani yake, hasa kuhusu haki za kibinadamu na haki halali za watu wa Palestina.
Hivi karibuni duru zimedokeza kuwa, Harakati ya Ansarullah ya Yemen iko tayari kuchukua udhibiti wa eneo la kimkakati la Lango Bahari wa Bab al‑Mandab kama sehemu ya hatua za nguvu za Muqawama (Mapambano) za kuwaadhibu maadui walioanzisha hujuma ya kichokozi dhidi ya Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, duru za Ansarullah zimedokeza kuwa, tangu siku ya kwanza ya Vita vya Ramadhani vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, harakati hiyo ya Muqawama ya Yemen imekuwa katika hali ya tahadhari kamili na iko tayari kuingia katika uwanja wa mapambano.
4343108