Dkt. Masoud Pezeshkian, amesisitiza msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuimarisha umoja wa ulimwengu wa Kiislamu, huku akiishukuru Pakistan kwa juhudi zake katika upatanishi na kuweka usitishaji wa mapigano. Ameongeza kuwa Tehran inataka amani ya kudumu na utulivu wa kweli katika eneo, na inasisitiza juu ya haki za taifa la Iran kulingana na misingi ya sheria za kimataifa.
Rais Pezeshkian ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Jenerali Asim Munir, Kamanda wa Jeshi la Pakistan ambapo ametoa shukrani kwa mchango wa kamanda huyo pamoja na Waziri Mkuu wa Pakistan, Bw. Shehbaz Sharif, katika mchakato wa upatanishi baina ya Iran na Marekani na kurahisisha utekelezwaji wa usitishaji vita.
Rais aliendelea kusisitiza msimamo wa kimsingi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu ulimwengu wa Kiislamu, na kuonza kuwa : Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayaona mataifa yote ya Kiislamu kama ndugu, mtazamo unaotokana na Sira ya Mtume Muhammad (SAW). Hata hivyo, amesema hatua za hivi karibuni za kulenga vituo vya kijeshi vya Marekani katika baadhi ya nchi za eneo zimefanyika kulingana na mahitaji ya kujilinda na kama jibu kwa mazingira yaliyoilazimishwa Iran.
Dkt. Pezeshkian ameongeza kuwa chanzo cha migogoro na kutokuwa na utulivu katika eneo mara nyingi kinahusishwa na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel zinazolenga kuleta mpasuko kati ya mataifa ya Kiislamu. Amesema kwamba Umma wa Kiislamu unapaswa kusimama pamoja ili kuzuia utawala huo kutumia ardhi za Kiislamu dhidi ya Waislamu wenyewe.
Rais aidha amebainisha kuwa watu wa Iran hawaiamini Marekani kutokana na ukiukaji wa mara kwa mara wa ahadi, mashambulizi wakati wa mazungumzo, na mauaji ya viongozi. Amesema kuwa licha ya hali hizi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikitegemea mahusiano ya kindugu na mataifa rafiki kama Pakistan, imeingia katika mchakato huu, ila bila shaka itaendelea kulinda maslahi ya taifa lake kwa uthabiti.
Katika mazungumzo hayo, Jenerali Asim Munir amesisitiza umuhimu wa juhudi zinazoendelea za kuhitimisha vita, na kusema: Tunaamini kwamba makubaliano yanaweza kupatikana hivi karibuni, na tunasisitiza kuwa vita hivi havina matokeo mengine ila uharibifu na hasara.
Kamanda huyo wa Jeshi la Pakistan pia aliwasilisha taarifa kuhusu mchakato wa mazungumzo na akabainisha matumaini kwamba katika siku zijazo kutapatikana makubaliano na vita vitamalizika.
4346861