IQNA

Israel yawapiga marufuku wahubiri wa Kiislamu Wapalestina kuingia Msikiti wa Al‑Aqsa

13:12 - May 07, 2026
Habari ID: 3482211
IQNA – Utawala dhalimu wa Israel umewapiga marufuku wahubiri wawili mashuhuri wa Kiislamu wa Palestina kuingia katika Msikiti wa Al‑Aqsa  jijini Al Quds (Jerusalem) kwa kipindi cha miezi sita.

Polisi wa utawala wa Israel katika mji wa al‑Quds wametoa uamuzi wa kumfukuza Sheikh Raed Salah na Sheikh Kamal Khatib kutoka eneo la Msikiti wa Al‑Aqsa na viwanja vyake kwa muda wa miezi sita, kuanzia Aprili 27, 2026 hadi Oktoba 27, 2026.

Uamuzi huo, uliotiwa saini na kamanda wa polisi wa eneo la al‑Quds, Afshlom Bild, unatokana na mamlaka anayodaiwa kupewa chini ya amri za polisi za utawala huo zilizowekwa mwaka 1971, kwa kisingizio cha “kulinda usalama na utulivu wa umma.”

Maamuzi hayo yanaeleza kuwa kuna “marufuku ya kuingia kwa masheikh hao wawili katika viwanja vya Msikiti wa Al‑Aqsa au kuwepo humo, isipokuwa kwa kupata kibali maalumu na cha moja kwa moja kutoka kwa kamanda wa polisi.”

Akizungumzia uamuzi huo, Sheikh Kamal Khatib alikataa hatua hiyo, akiitaja kuwa ni sehemu ya “msako unaoendelea” tangu kupigwa marufuku kwa harakati ya Kiislamu mwaka 2015, na kuashiria kuwa sababu za usalama zilizotolewa “hazina hoja za msingi.”

Aliongeza pia kuunganisha muda wa uamuzi huo na mfululizo wa kesi anazokabili tangu 2021 zinazohusiana na tuhuma za uchochezi, akisisitiza msimamo wake kwamba ataendelea kushikamana na misimamo yake licha ya hatua zinazochukuliwa dhidi yake.

Hatua hii ni mwendelezo wa masharti na vizuizi mbalimbali ambavyo utawala wa Israeli umekuwa ukiweka dhidi ya masheikh hao katika miaka ya karibuni, vikiwemo maagizo ya mara kwa mara ya kuwafukuza kutoka Msikiti wa Al‑Aqsa pamoja na hatua nyingine za kuwazuia.

Sheikh Raed Salah, aliyewahi kuongoza harakati ya Kiislamu kabla ya kupigwa marufuku kwake, amekumbana mara nyingi na kukamatwa na kufukuzwa, huku Sheikh Kamal Khatib aliyekuwa Naibu Mkuu wa harakati hiyo, kwa sasa akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uhuru chini ya Kamati ya Ufuatiliaji ya Juu, naye akikabiliwa na hatua zinazofanana.

Hatua hii inaakisi mwendelezo wa sera zinazoathiri uwezo wa  Waislamu kufika  katika Msikiti wa Al‑Aqsa, eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu.

3497375

Habari zinazohusiana
captcha