Kwa mujibu wa ripoti ya Al Jazeera, Kituo cha Qur’ani cha Al-Nour kinaendelea kutoa programu za kielimu na mwongozo wa kiroho. Hata hivyo, wasimamizi wa kituo hicho wanasisitiza kuwa kuendelea kwa shughuli hizo kunategemea sana upatikanaji wa mahitaji ya msingi kama vile nakala za Qur’ani, feni (za kupunguza joto), maji, na vifaa muhimu vya kuwasaidia wanafunzi katika hali ngumu ya sasa.
Kituo hicho kinatoa programu mbalimbali, zikiwemo za kuhifadhi Qur’ani, mihadhara ya kidini, programu za kitaaluma, kambi za kiangazi, na vikao vya usomaji Qur’ani kwa wazee. Pia, kinatoa mafunzo ya usomaji Qur’ani kwa watoto na watu wazima. Aidha, kituo kinaendesha programu ya “Chipukizi wa Qur’ani” (Quranic Buds), ambayo inajumuisha mafunzo ya adabu, maadili, fikihi, na hadithi kwa wasichana wa rika zote, kuanzia shule ya msingi hadi ngazi ya chuo kikuu.
Wasimamizi wa kituo wameiambia Al Jazeera kuwa vita vimeleta hali halisi mpya inayolazimisha umakini mkubwa zaidi katika kukuza thamani za Kiislamu na kuimarisha uhusiano wa wanafunzi na Qur’ani Tukufu. Walibainisha kuwa kituo kinatoa kozi za kanuni za usomaji Qur’ani (Tajwid) kwa wanawake na watoto, na kinapokea wanafunzi wa kiume kati ya umri wa miaka sita na tisa, na wanafunzi wa kike wa umri wowote kuanzia miaka mitano hadi tisini.
Uongozi wa kituo hicho ulieleza kuwa wanafunzi huanza siku yao saa 2 asubuhi, wakitoka katika makazi yao ya muda, mahema, au mashule yaliyohifadhiwa, na kwenda msikitini kushiriki katika programu ya kila siku inayodumu hadi saa 8 mchana. Programu hiyo inajumuisha vikao vya usomaji na kuhifadhi Qur’ani. Wasimamizi walisisitiza kuwa saa hizi ndefu zinahitaji uwepo wa chakula kidogo (vitafunio) au motisha nyingine ili kuwasaidia wanafunzi kuendelea na juhudi zao za kuhifadhi.
Kutokana na uhaba Misahafu au nakala za Qur’ani, kituo kimelazimika kutumia mbinu ya mafunzo ya mdomo. Waalimu husoma kwa kutumia kumbukumbu zao, wakianza na Juzuu ya 30 na kisha kuendelea na sehemu nyingine, ili kuhakikisha elimu inaendelea kutolewa licha ya ufinyu wa rasilimali.
Maafisa wa kituo wanathibitisha kuwa nakala nyingi za Qur’ani zilizopo msikitini zimechanika au kuchakaa, na baadhi zimeokolewa kutoka katika vifusi vya majengo yaliyobomolewa ili zitumike katika kuwafundisha wanafunzi. Wanasisitiza kuwa lengo lao kuu ni kulinda utambulisho wa kidini na kupandikiza mafundisho ya Qur’ani katika nyoyo za kizazi kipya, licha ya mazingira magumu ya vita.
Wasimamizi wa kituo wanawaomba wafadhili kutoa feni za kupunguza joto kali ndani ya msikiti. Pia, wanaomba maji ya kunywa, nakala za Qur’ani, hijabu, na mavazi yanayostahili kwa wanafunzi ili waweze kuhudhuria madarasa ya Qur’ani katika hali bora zaidi.
“Kufika msikitini kumegeuka kuwa kazi nzito,” anasema mmoja wa waalimu. Anaeleza kuwa kituo hicho kilianzishwa kwa rasilimali duni, na msikiti huo bado ni muundo wa muda ( makeshift) ambao hauna hata huduma za msingi kabisa. Anaongeza kuwa wanafunzi wana umri kuanzia miaka 5 hadi 19, na wazee pia huhudhuria. Kituo pia kinahitaji misala na mavazi kwa ajili ya watoto.
Anabainisha kuwa watoto na familia zao wanakabiliwa na hofu ya daima wanapojaribu kufika msikitini kutokana na mabomu ya kila mara. Hata hivyo, hali hii haijawazuia kuendelea na masomo yao. Anasema kuwa waalimu wanaendelea kuwasaidia wanafunzi kwa rasilimali chache walizonazo, licha ya shinikizo la kisaikolojia na kiuchumi linaloathiri kila mtu.
Anaeleza kuwa mabomu ya kila siku yanafanya maisha kuwa magumu zaidi kila uchao, lakini kituo kinaendelea na shughuli zake, kikiamini katika umuhimu wa kufundisha Qur’ani. Ana matumaini kuwa juhudi hii itaendelea kwa msaada mpana zaidi.
Mwanafunzi mmoja anasema kuwa furaha yake kuu ni kwenda msikitini kuhifadhi Qur’ani na Hadithi, na kujifunza kanuni za usomaji. Hata hivyo, anabainisha kuwa kufika msikitini imekuwa kazi ngumu kutokana na kuharibiwa kwa barabara.
Anasisitiza kuwa umbali mrefu na ugumu wa usafiri unazidisha mateso ya wanafunzi, hasa wale wanaotoka maeneo ya mbali. Hata hivyo, anasisitiza kuwa licha ya dhiki hizo wanazokumbana nazo, wanahisi utulivu na furaha kubwa pindi tu wanapofika kwenye vikao vya kuhifadhi Qur’ani.
Mwanafunzi anahitimisha kwa kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwapa misaada ya kiroho na kimaada wanafunzi wa kituo hicho. Anaamini kuwa hata misaada ya kiasi kidogo kabisa inatosha kuwatia moyo na kuwapa matumaini baada ya kupoteza wapendwa wao na kupitia mateso makali. Aidha, anatoa wito wa kukomeshwa kwa vita na kurejeshwa kwa amani ya kudumu, ili wakazi wa Ukanda wa Gaza waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida na ya utulivu.
Ukanda wa Gaza umekuwa ukikabbiliwa na vita vya mauaji ya kimbari vya utawala haramu wa Israel tokea Oktoba 7 2023 na hadi sasa utawala huo katili umeua Wapalestina wasiopungua 73,000 wengi wakiwa ni wanawake na watoto huku zaidi ya asilimi 90 ya eneo hilo likiwa limeharibiwa katika vita hivyo.
3498218