IQNA

Kisomo cha Surat Yusuf: Njia ya ufanisi na lakabu ya “Sultan al-Qurra” kwa Sheikh al-Sayyid Saeed

21:55 - May 31, 2026
Habari ID: 3482308
IQNA – Wengi wanaamini kuwa kurekodiwa kwa Surat Yusuf kulikuwa mgeuko wa kweli katika maisha ya Sheikh al-Sayyid Saeed, na mafanikio hayo makubwa yakamfanya ajipatie umaarufu na hatimaye kunyakua lakabu inayostahiki ya “Sultan al-Qurra” (Mfalme wa Wasomaji Qur’ani).

Hii ni lakabu ambayo ameibeba miongoni mwa wasomaji wa Misri hadi leo.

Sheikh al-Sayyid Saeed alikuwa miongoni mwa nguzo muhimu katika nyanja ya usomaji wa Qur’ani Tukufu nchini Misri na ulimwenguni mwa Kiislamu kwa ujumla.

Alizaliwa tarehe 7 Machi 1943 katika kijiji cha Meit Marja Salsil, sehemu ya mji wa Jamaliyah katika mkoa wa Dakahlia, Misri. Alikulia katika familia ya kipato cha chini yenye watoto tisa, akiwa ndiye mdogo kuliko wote. Tangu utotoni, alikuwa na kipaji cha kipekee cha sauti.

Sheikh Saeed aliihifadhi Qur’ani akiwa na umri wa miaka 9. Safari yake ya Qur’ani ilianza katika Maktab (shule ya Qur’ani) ya kijijini kwao, akijifunza chini ya Sheikh Abdul Mahmoud Othman. Kutokana na kipaji chake cha ajabu cha usomaji, umaarufu wake ulienea katika mkoa mzima, na baadaye akasafiri katika nchi nyingi duniani kwa ajili ya kusoma Qur’ani.

Saeed aliacha shule akiwa mdogo kutokana na hali ngumu ya kiuchumi. Hata hivyo, alipata njia yake katika ulimwengu wa usomaji wa Qur’ani kupitia sauti yake ya kupendeza na uwezo wake wa kumudu Maqamat (misingi ya sauti) kwa kusikiliza tu, bila ya mafunzo rasmi. Huyu “Sultan al-Qurra” wa Misri aliwavutia watu waliomzunguka, na jina lake kama msomaji mahiri lilienea kila mahali.

Sheikh Saeed alikuwa akisoma Qur’ani bila ya kudai ujira wowote. Alikuwa akisema: “Naisoma Qur’ani kwa ajili ya mapenzi yangu kwake, si kwa ajili ya fedha. Aya za Mwenyezi Mungu hazina thamani ya kuuzwa.”

Qari huyu wa Misri alisoma Qur’ani katika nchi nyingi duniani, ikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu, Iraq, Lebanon, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jamhuri ya Azerbaijan, na Uswisi.

Alijulikana kwa sauti yake tulivu na utendaji wake wa kiufundi na kiroho. Aliwahi kusoma Qur’ani sambamba na baadhi ya magwiji wakubwa wa usomaji wa Qur’ani nchini Misri, kama vile Sheikh Muhammad Siddiq Minshawi, Mustafa Ismail, Abdel Fattah Al-Shasha’i, Mahmoud Ali Al-Banna, na Sheikh Abu Al-Ainain Shuaisha; hatua iliyompatia nafasi ya juu miongoni mwa wasomaji wakubwa wa Kitabu Kitukufu.

Sheikh Saeed aliinua bendera ya Qur’ani Tukufu katika majukwaa ya kimataifa na kupata pongezi tele pamoja na mapenzi makubwa kutoka kwa wasikilizaji wake.

Msomaji huyu wa Misri pia alijulikana kwa mtindo wake wa kipekee katika kusoma Surat Yusuf, mtindo ambao uligeuka kuwa kama shule ya kipekee katika sanaa ya usomaji wa Qur’ani.

Alistahiki kabisa kuitwa Sultan al-Qurra kutokana na utendaji wake usio na kifani, hasa katika usomaji wake wa kuvutia na wenye mguso wa kiroho wa Surat Yusuf, ambao wengi huuchukulia kuwa ndio usomaji wake bora zaidi kuwahi kurekodiwa. Katikati ya miaka ya 1990, sauti yake ilitawala soko la Misri, na katika kipindi hicho, kanda zake za kaseti ziliuzwa kwa wingi mno, kiasi kwamba sauti yake ya Qur’ani ilisikika kila mahali—majumbani, madukani, na hata katika vyombo vya usafiri wa umma jijini.

Wengi wanaamini kuwa kurekodi kwake Surat Yusuf kulikuwa mgeuko mkubwa katika maisha yake; mafanikio hayo makubwa ndiyo yaliyompatia umaarufu na kumstahilishia lakabu hiyo ya Sultan al-Qurra.

Alikuwa na nafasi kubwa katika Chama cha Wasomaji na Wahifadhi wa Qur’ani cha Misri, na alikuwa mwenyekiti wa matawi ya chama hicho katika mikoa ya Dakahlia na Damietta. Alichangia pakubwa katika kulea kizazi cha wasomaji waliofuata nyayo zake katika kuimudu sanaa ya usomaji na kuutumikia Qur’ani Tukufu.

Sheikh al-Sayyid Saeed aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake tarehe 24 Mei 2025 akiwa na umri wa miaka 82, baada ya muda wa kupambana na maradhi. Mwenyezi Mungu Amrehemu

Hapa chini unaweza kusikiliza usomaji wake wa aya za 19 hadi 31 za Surat Yusuf:

4354330

Kishikizo: qurani tukufu qari misri
captcha