IQNA

Papa asikiliza Biblia na Qur’ani katika mkutano wa kidini Beirut

20:02 - December 02, 2025
Habari ID: 3481603
IQNA – Papa Leo XIV amehudhuria mkutano wa dini mbalimbali uliofanyika katika Uwanja wa Mashahidi jijini Beirut, ambapo walikusanyika mapatriaki wa Kikristo wa Lebanon pamoja na viongozi wa Kiroho wa Kiislamu wa madhehebu ya Sunni na Shia na halikadhalika dini ya Druze chini ya hema moja.

Baada ya kusikiliza nyimbo na masomo kutoka Biblia na Qur’ani Tukufu, Papa Leo XIV alisifu utamaduni wa Lebanon wa kustahimili dini tofauti, akiuona kama taa ya “zawadi ya amani ya Kiungu” katika eneo hilo.

Katika hotuba yake alisema: “Katika zama ambapo kuishi pamoja huonekana kama ndoto ya mbali, watu wa Lebanon, wakiwa wamekumbatia dini tofauti, wanasimama kama kumbusho lenye nguvu kwamba hofu, kutoaminiana na upendeleo havina neno la mwisho, bali mshikamano, maridhiano na amani vinawezekana.”

Ujumbe wa Papa ulisisitiza umuhimu wa Lebanon na Wakristo wake kwa Kanisa Katoliki, akirejelea kauli maarufu ya Mtakatifu Yohane Paulo II aliyosema Lebanon si nchi pekee bali ni ujumbe wa uhuru kwa ulimwengu mzima.

Mufti Mkuu wa Sunni wa Lebanon, Abdul-Latif Derian, alimkaribisha Papa katika mkutano huo na kukumbusha uhusiano mwema uliowekwa na mtangulizi wake, Papa Francis. Alinukuu tamko la pamoja la mwaka 2019 kuhusu Udugu wa Kibinadamu lililosainiwa na Francis na Imam Mkuu wa Al-Azhar, Sheikh Ahmed al-Tayeb. “Lebanon ni ardhi ya ujumbe huu,” alisema Derian.

Mwisho wa mkutano huo, viongozi wa kidini walipanda mche wa mzeituni kama alama ya amani.

Papa alipokelewa kwa shangwe na viongozi wa kiroho wa Lebanon katika siku yake ya kwanza ya ziara, ambapo mabango yenye picha yake yalipamba barabara kuu za Beirut, na maelfu ya wananchi wa kawaida wakavumilia mvua ya asubuhi ili kusimama kando ya barabara ya msafara wake.

3495597

Habari zinazohusiana
captcha