
Katika barua hiyo, Ayatullah Sayyid Mostafa Mohaqeq Damad amesifu uthabiti wa Papa katika kusimama kidete dhidi ya wapiga ngoma wa vita, akauona msimamo huo kuwa ni ishara ya mgongano wa baina ya “urahibuni wa kweli wa kiroho” na siasa zilizochafuliwa.
Ameandika: “Baada ya barua yangu ya Machi 20, 2026 niliyokuandikia kuhusu mashambulizi ya kidhulma dhidi ya Iran, na kuonyesha shukrani zangu kwa wema wako, niliona ni wajibu kurudia kutoa shukrani kwa msimamo wako wa kutafuta haki na kukataa vitendo vya ukatili. Kusimama kwako kwa ujasiri dhidi ya wapiga ngoma wa vita kumeendelea kufunua hitilafu kati ya kiroho halisi na siasa zilizogubikwa na uchafu.”
Ameongeza kuwa: “Katika wakati huu nyeti, kusikia sauti za wasaidizi wako waheshimiwa, hasa kauli za wazi za Mheshimiwa Askofu Mkuu Timothy Broglio, Askofu wa Jeshi la Marekani, na Kardinali Robert McElroy, kumeleta faraja kwa wanaotafuta amani. Ukweli kwamba viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki, wakitegemea misingi ya maadili na ‘Nadharia ya Vita vya Haki,’ wametoa msimamo wa kishujaa kuhusu kutokubalika kwa vita hivi vilivyolazimishwa, ni dalili ya uhai wa maadili ndani ya mwili wa Kanisa. Tafadhali wafikishie shukrani zangu za dhati.”
Mwanachuoni huyo wa Kiislamu kutoka Iran ameongeza kuwa:
“Ni jambo la kusikitisha mno kuwa tunashuhudia misimamo isiyo ya haki ya baadhi ya serikali ambazo zimechochea moto wa vita dhidi ya Iran kwa wazi wakivunja taratibu za kimataifa. Mashambulizi haya yamesababisha uharibifu mkubwa wa makazi ya watu wanaotafuta amani, uharibifu wa mabaki ya kale na urithi wa tamaduni, ambavyo ni vitambulisho vya ustaarabu wa mwanadamu, na pia yamelenga vituo vya kielimu na kusababisha kumwagika kwa damu ya maelfu ya watu wasio na hatia, hasa wanafunzi wadogo.”
“Historia na dhamiri iliyozinduka ya wanadamu kamwe haitasahau kuwa madhalimu, kwa kutaka kufunika aibu ya vitendo vyao, wamethubutu hata kutusi alama za kimungu na kuwadhalilisha waletezi wa uadilifu. Lakini vitendo hivi vibaya vyenyewe ni ushahidi wa nguvu ya maneno ya mamlaka yako tukufu, yanayowapa moyo mabilioni ya watu wanaoota dunia isiyo na ubaguzi wala ukatili.”
“Katika mafunzo ya dini za tauhidi, amani ni matunda ya mti wa usafi wa moyo na uchaji. Mimi ambaye kwa zaidi ya miongo mitatu nimebahika kufanya mijadala na viongozi mashuhuri wa dini za Ibrahimu, na nimekuwa na mawasiliano na Vatican tangu enzi za Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, nikikumbuka hotuba yangu katika Sinodi ya Amani kwa mwaliko wa Baba Mtakatifu Benedict wa Kumi na Sita, na baadaye mbele ya Baba Mtakatifu Francis nikiendeleza umuhimu wa kulinda mazingira."
“Ingawa hadi sasa sijapata fursa ya kukutana na Baba Mtakatifu (Papa Leo), mimi kama mwanafunzi na msomi wa Kishia, naona misimamo yenu ya kurudia kukataa kumwagika kwa damu kuwa ni kitovu muhimu katika historia ya leo. Ukweli wa maneno yenu hautafunikwa na kelele za wale ambao majina yao yanakumbusha tu kuporomoka kwa maadili.”
Mwisho wa barua hiyo, Ayatullah Mohaqeq Damad akaomba dua kwa ajili ya “ustahimili na mafanikio zaidi kwa Baba Mtakatifu na kwa makardinali na maaskofu wote wanaopenda amani katika huduma yao kwa mwanadamu.”
3497258