
Trump alimkosoa vikali Papa Leo XIV, akidai kuwa kuchaguliwa kwake kuongoza Kanisa Katoliki duniani kulichangiwa na ushawishi wa Marekani, huku akionesha kutoridhishwa na msimamo wa Papa wa kupinga hatua za Marekani dhidi ya Venezuela pamoja na mtazamo wake mpana wa kupinga vita.
Katika chapisho kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alidai kuwa “Kama nisingekuwa katika Ikulu ya White House, Leo asingekuwa Vatican."
“Leo anapaswa kushukuru kwa sababu, kama kila mtu anavyojua, hakuwa kwenye orodha yoyote ya kuwa Papa, na aliwekwa tu hapo na Kanisa kwa sababu alikuwa Mmarekani, na walidhani hiyo ndiyo njia bora ya kushirikiana na Rais Donald J. Trump,” aliongeza.
Trump pia alimwelezea papa huyo kuwa eti ni dhaifu katika masuala ya uhalifu na silaha za nyuklia, kauli ambazo zinaonekana kuhusiana na ukosoaji wa hadhara wa papa kuhusu hatua za kijeshi.
Ukosoaji wa rais wa Marekani umeibuka wakati ambapo Papa Leo XIV alitoa mahubiri yenye msisitizo mkubwa wa kupinga vita katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro tarehe 11 Aprili.
“Kifo huwafanya watumwa wale waliompa mgongo Mungu aliye hai, wakijigeuza wenyewe na nguvu zao kuwa sanamu bubu, kipofu na kiziwi. Imetosha basi kuabudu madaraka na mali! Imetosha basi kuonesha nguvu kwa majivuno! Imetosha basi kueneza vita!” alisema kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.
Aidha wakati wa sala ya kila wiki ya Angelus katika Uwanja wa Mtakatifu Petro huko Vatican, mwezi Machi Papa Leo alisema dunia haina haki ya kubaki katika hali ya kutojali mateso ya raia.
“Hatuwezi kukaa kimya mbele ya mateso ya watu wengi, wahanga wasio na ulinzi wa mizozo hii. Kinachowaumiza wao, kinaumiza ubinadamu wote,” alisisitiza.
Papa Leo amesema kuwa matukio yanayoendelea Mashariki ya Kati yanamletea wasiwasi mkubwa.
Waangalizi wanaeleza kuwa mahubiri ya hivi karibuni ya Pap pia yamegusia moja kwa moja matukio ya katika Mashariki ya Kati pamoja na ukosoaji wa sera za serikali ya Marekani.