IQNA

Wamisri Washinda Nafasi za Juu katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Port Said

13:10 - February 03, 2026
Habari ID: 3481884
IQNA — Toleo la tisa la Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur’ani na Ibtihal ya Port Said limehitimishwa, ambapo washiriki kutoka Misri wameibuka kidedea kwa kushinda nafasi ya kwanza katika makundi yote matatu ya mashindano hayo.

Kwa mujibu wa IQNA, likinukuu taarifa za mashindano ya 9 ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur’ani na Dua za Kidini (Ibtihal), hafla ya kufunga mashindano hayo ilifanyika katika Msikiti wa Abbasi, mjini Port Said, Misri, Jumatatu alasiri (Februari 2), kwa ushiriki wa maafisa wa serikali ya Misri pamoja na idadi kubwa ya wanazuoni na viongozi wa kidini na kiutawala, kama ilivyoripotiwa na Al-Bawaba News.

Baraza la majaji lilimtangaza Ahmad Ali Youssef Saif, mzaliwa wa nchi mwenyeji, kuwa mshindi wa nafasi ya kwanza katika kipengele cha kuhifadhi Qur’ani kwa riwaya mbili, huku Ibrahim Idris Ibrahim kutoka Libya akishika nafasi ya pili na Jihad Miteb Al-Maliki kutoka Saudi Arabia akichukua nafasi ya tatu.

Katika kipengele cha sauti nzuri (husn al-sawt), Khaled Nasser Sabah kutoka Misri aliibuka mshindi wa kwanza, akifuatiwa na Murshed Salendab kutoka Ufilipino katika nafasi ya pili, na Falah Zalif kutoka Iraq katika nafasi ya tatu.

Aidha, kipengele cha Ibtihal kilishuhudia umahiri wa Mohammed Yasser kutoka Misri, aliyeshinda nafasi ya kwanza, huku Hamza Al-Qasimi kutoka Morocco na Majd Ghamdan kutoka Yemen wakishika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.

Habari inayohusiana:

Mashindano hayo yalianza Januari 31 katika mji wa bandari wa Port Said, yakishirikisha wawakilishi kutoka mataifa 30 duniani. Jumla ya wasomaji 42 wa Qur’ani, wahifadhi na waimbaji wa Ibtihal walishindania tuzo za juu.

Mashindano ya mwaka huu yalipewa jina la marehemu msomaji mashuhuri wa Misri, Sheikh Mahmoud Ali Al-Banna, kwa heshima ya mchango wake mkubwa na wa kudumu katika kuhudumia Qur’ani Tukufu.

4332048

Habari zinazohusiana
captcha